1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel ahimiza uwekezaji barani Afrika

 Harrison Mwilima19 Novemba 2019

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amehimiza hatua za kutambua fursa na pia changamoto zilizopo barani Afrika, hivyo kuhamasisha uwekezaji katika nchi hizo.

https://p.dw.com/p/3TKXo
Deutschland Berlin | Konferenz Compact with Africa | Angela Merkel, Bundeskanzlerin | Gruppenbild
Picha: Reuters/F. Bensch

Mkutano wa kilele wa uwekezaji wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia za kundi la G20 ulioangazia wafanya biashara wa Kijerumani wanaowekeza katika nchi za Afrika zilizopo kwenye mpango unaofahamika kama Compact with Africa, umefanyika leo jijini Berlin chini ya uongozi wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. 

Mkutano huo wa tatu wa kilele unaoleta nchi 12 za Afrika ambao ni wanachama wa Compact with Africa umewaleta pamoja marais na viongozi mbali mbali kutoka nchi hizo 12 ambazo ni: Benin, Burkina Faso, Ivory Coast, Misri, Ethiopia, Ghana, Guinea, Morocco, Rwanda, Senegal, Tunisia na Togo.

Mpango huo wa Compact with Africa na nchi hizo 12 ulianzishwa na Ujerumani wakati nchi hiyo ilipochukua urais wa kundi la  G20 mwaka 2017 kama njia ya kutambua fursa na pia changamoto zilizopo barani Afrika, hivyo kuhamasisha uwekezaji katika nchi hizo kutoka Ujerumani na nchi za G20 kwa ujumla. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza ni kwa nini Ujerumani ilihamasisha mpango huo katika G20.

"Sote tunakubaliana kwamba ukiachilia misaada ya kimaendeleo, inabidi kusaidia nchi hizo zijiendeleze kiuchumi na hiyo ndio sababu ya sisi kuhamasisha mpango huu wa Compact with Afrika katika Urais wetu wa nchi za G20 mwaka 2017 na dhumuni letu kuu lilikua ni kuhakikisha uwekezaji binafsi kuelekea nchi wanachama unaongezeka."

Rais wa rwanda Paul Kagame (Kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (Kulia)
Rais wa rwanda Paul Kagame (Kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (Kulia) Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Nchi pekee ya kutoka Afrika Mashariki inayoshiriki katika mpango huo wa Compact with Afrika ni Rwanda. Rais wa nchi hiyo Paul Kagame alieleza mifano ya uwekezaji kutoka makampuni ya Kijerumani tokea mpango wa Compact with Afrika ulipoanza.

"Mfano ni ushirikiano Rwanda iliyoupata kutoka Volkswagen, Siemens nayo sasa inakuja pamoja na SAP na tunataka kuendelea kuona uwekezaji zaidi kutoka Ujerumani, kutoka Ulaya na nchi za G20 katika ushirikiano huu ulioundwa." Amesema rais Kagame.

Katika mkutano huo, pia mikataba mipya mikubwa ya uwekezaji kutoka makampuni makubwa ya Kijerumani kuelekea nchi hizo zinazoshiriki katika mpango wa Compact with Africa, ilisainiwa.