1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kane: Ni sharti tushinde mechi zilizosalia kabla mapumziko

27 Novemba 2023

Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry Kane kwa sasa ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao 18, mabao mawili zaidi ya mfungaji bora wa msimu wote uliopita.

https://p.dw.com/p/4ZUai
Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga FC Köln v Bayern München | Harry Kane
Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry KanePicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Katika mechi ya Ijumaa walipopata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya FC Cologne, Kane ndiye aliyekuwa mfungaji wa bao hilo na akaipelekea Bayern kuwa kileleni ingawa kwa masaa machache.

Muingereza huyo anasema safari bado ni ndefu ila matarajio yake ni kumaliza mwaka huu wakiwa kileleni mwa Bundesliga.

"Bila shaka bado kuna mechi nyingi sana za kucheza, mechi nyingi ngumu. Bayer Leverkusen wameuanza msimu vyema kwa hiyo bado safari ni ndefu. Tunachostahili kufanya ni kucheza vyema katika kila mechi na kuanzia sasa hadi kipindi cha mapumziko mwishoni mwa Desemba, tunastahili kujaribu tu kushinda mechi nyingi ipasavyo," alisema Kane.

Katika mechi hiyo dhidi ya FC Cologne, Bayern walipata nafasi nyingi na waliudhibiti mchezo pakubwa ila hawakuzitumia vyema nafasi hizo, dhidi ya timu ambayo kwa sasa inachungulia kushuka daraja.

Kocha Thomas Tuchel lakini hana mashaka kwamba vijana wake watayarekebisha makosa yao na kuzitumia vyema nafasi zao kuelekea mechi ya mwishoni mwa wiki watakapochuana na Union Berlin.

"Kwa kwaida hawa vijana wanao uwezo wa kuzitumia nafasi wanazopata, leo hii haikuwa hivyo, wakati mwengine haya hutokea. Kipindi cha pili tuliudhibiti mchezo kikamilifu, hatukuwapa nafasi yoyote kwasababu tulikuwa tumeidhibiti mechi kikamilifu, hatukukubali mashambulizi ya kushtukiza. Tulikuwa tumejipanga vyema , tukacheza vyema na tulistahili kushinda," alisema Tuchel.

Ligi Kuu ya Ujerumani RB Leipzig - Bayern München
Kocha wa Bayern Munich Thomas TuchelPicha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Bayern watakuwa na nafasi nzuri ya kuingia uongozini mwa Bundesliga iwapo watapata ushindi kwenye mechi hiyo na Union hasa ukizingatia Bayer Leverkusen watakuwa nyumbani kuwakaribisha Borussia Dortmund, hivyo dua za Bayern zitakuwa hao watani wao wa tangu jadi, Dortmund walizamishe jahazi la Leverkusen.

Vyanzo: AP/Reuters