Kampuni za magari Ujerumani zakumbwa na kashfa nyingine
29 Januari 2018Utafiti huo ulifanywa na chuo kikuu cha Aachen na kuidhinishwa na shirika linalofahamika kama European Research Group on Environment and Health in the Transport Sector EUGT, linalofadhiliwa na makampuni ya magari ya Volkswagen, Daimler na BMW. Ufichuzi huu wa kushtua umekuja baada ya hapo mwishoni mwa wiki iliyopita, kuripotiwa kwamba majaribio ya namna hiyo yalifanywa kwa ngedere.
Gazeti la New York Times la nchini Marekani liliripoti Jumamosi iliyopita kuwa kituo cha utafiti wa maradhi yanayohusiana na pumzi cha Lovelace (LRRI) chenye makao yake New Mexico nchini Marekani kilipewa kazi na shirika la EUGT kuanda majaribio ambamo ngedere 10 waliwekwa katika chumba kisichoingiza au kutoa hewa na kuvutishwa moshi kutoka kwenye gari la dizeli la VW aina ya Beetle.
Yote hayo yanaripotiwa kutokea kati ya mwaka 2012 na 2015, na makampuni hayo ya magari yaliamua mwishoni mwa mwaka 2016 kuivunja EUGT, ambayo hatimaye ilikuja kufungwa kabisaa mwaka uliopita.
Hasira zaongezeka
Kwa mujibu wa magazeti ya Ujerumani ya Stuttgarter Zeitung na Süddeutsche Zeitung, utafiti huo ulijikita katika uvutaji wa muda mfupi wa naitrojeni dioksidi kwa watu wenye afya. Kisha hospitali ya chuo kikuu cha Aachen iliwapima watu 25 waliovuta gesi hiyo kwa viwango tofauti kwa masaa kadhaa.
Wanasiasa nchini Ujerumani wamelaani vikali kitendo hicho, huku makampuni yaliotajwa yakijitenga na utafiti huo na kusema mbinu iliotumiwa na EUGT wakati huo haikuwa sahihi.
Waziri wa usafiri wa Ujerumani Christian Schmidt, amesema kupitia msemaji wake kwamba utafiti huo haukufanyika kwa sababu zozote za kiuchumi bali kwa faida binafsi za makampuni, na kwamba kampuni hizo zimetakiwa kutoa majibu ya haraka na ya kina.
"Tume ya uchunguzi ya wizara itakuwa na kikao maalumu kutathimini iwapo kuna kesi nyingine zozote. Majaribio kama hayo kwa wanyama na binadamu yanapaswa kukomeshwa mara moja," alisema Ingo Strater wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Berlin.
Msemaji wa kansela Angela Merkel Steffen Seibert, amesema hasira walizo nazo watu wengi zinaeleweka kabisaa, na kuongeza mambo kama hayo hayawezi kwa njia yoyote ile kuwa na uhalali wa kimaadili.
"Kwa mujibu wa kinachojulikana kwa umma, hasira wanazosikia watu wengi zinaeleweka kabisaa. Majaribio haya kwa ngedere na binadamu hayawezi kwa namna yoyote ile kuwa na uhalali wa kimaadili. Na yanaibua maswali mengi kwa wale waliohusika na utafiti huo - na maswali haya yanapswa kujibiwa haraka," alisema Seibert.
Kampuni zajitenga na mbinu za EUGT
Ikijibu tuhuma hizo kampuni ya Volkwagen imesema katika taarifa kuwa wanaamini mbinu za kisayansi zilizocgaguliwa wakati huo hazikuwa sahihi. Kampuni ya Daimler ilisema siku ya Jumapili kuwa ilishtushwa na kiwango cha utafiti huo na namna ulivyofanyika, na kuongeza kuwa haikuwa na usemi kuhusu mbinu na hatua zilizochukuliwa na EUGT, na kwamba vilikuwa kinyume na kanuni za kimaadili za kampuni hiyo.
Stephan Weil, mwakilishi wa serikali ya jimbo la Lower Saxony, ambalo linamiliki hisa katika kampuni hiyo, kwenye bodi ya usimamizi ya kampuni hiyo, amesema bodi hiyo inaitaka VW kutoa taarifa haraka kuelezea nini hasa lilikuwa lengo la utafiti huo.
Mwandishi: Ulrike Quast/Wrede Insa/Iddi Ssessanga
Mhariri: Saumu Yusuf