1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Kampuni ya Woermann ilivyousafirisha ukoloni wa Ujerumani

21 Desemba 2023

Kampuni ya meli ya mfanyabiashara wa Hamburg, Adolph Woermann, ilianzia kupata faida kwa biashara ya ulevi Afrika ikaishia kwa kuwasafirisha wanajeshi makatili dhidi ya watu wa Herero na Nama nchini Namibia.

https://p.dw.com/p/4aRLJ
Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Kampuni ya Woermann ilikuwa nini?

Kampuni ya meli na biashara ya C. Woermann  — kutoka Hamburg — ilianzisha duka la kwanza mjini Douala, Kameruni, mnamo mwaka 1868. Ilifanya biashara kwenye Mwambao wa Afrika Magharibi.

Adolph Woermann alichukuwa biashara hii ya familia kutoka kwa baba yake, Carl Woermann, mwaka 1874. Kijana huyo mwenye tamaa aliamini Afrika lilikuwa soko la kuuzia bidhaa dhaifu za Kijerumani kama vile ulevi na pia mahala za kupata wafanyakazi rahisi kusaka malighafi za thamani kwa ajili ya viwanda vya Ujerumani.


Kwa nini Woermann alishinikiza Ujerumani iwe na makoloni?

Idadi kubwa ya makoloni yaliyoanzishwa na mataifa ya Ulaya ilimfanya Woermann ahofie kwamba yeye na wafanyabiashara wenzake wa Kijerumani wangelipoteza fursa ya masoko ya Afrika. Kansela Otto vo Bismarck alikuwa anasita kuanzisha makoloni, akiyaona kama ni anasa iliyo ghali sana kuigharamikia. 

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

Lakini jinsi ushindani wa Ulaya kwa masoko ya Afrika ulivyokuwa mkubwa, ndivyo pia ulivyokuwa ushawishi wa wafanyabiashara kama Woermann. Mnamo mwaka 1883, alipendekeza kuanzishwa kwa mahamiya katika Afrika Magharibi, akimshawishi Bismarck kwamba kufanya hivyo kungeionesha Ujerumani imefikia mahala pa kuwa kweli taifa kubwa. 


Woermann alikuwa na umuhimu gani kwenye mradi wa ukoloni?

Wanahistoria wakubwa wanajenga hoja kwamba ukoloni wa Ujerumani nchini Kameruni usingewezekana kama si Woermann. Mkataba wa Ujerumani na Douala wa Julai 1884 ulisainiwa na wafalme wa Douala na Akwa kumuhakikishia Woermann haki za ardhi na umiliki wa pekee wa biashara yote nchini Kameruni.

Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Woermann alikuwa mtu muhimu sana kwenye Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/1885 ambao uliyarasimisha madai ya ukoloni wa Ulaya. Biashara ya usafirishaji ya Woermann ilinawiri na kuwa mshirika mkuu wa utawala wa kibeberu wa Ujerumani.

"Mahamiya" yalikuwa mazuri kwa wafanyabiashara kwa sababu yalizilinda kampuni na masoko ya Kijerumani dhidi ya ushindani wa Ulaya, huku wakitegemea na kupata uungaji mkono wa jeshi la Ujerumani.


Kampuni ya Woermann ilifanya biashara gani?

Kiasi cha 60% cha biashara ya nje ya Ujerumani kwenye makoloni yake ilikuwa ni bidhaa za ulevi. Ili kuyalinda makoloni hayo dhidi ya uasi wa wenyeji na mataifa mengine makubwa ya Ulaya, silaha zilifuatia.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

Hili liliwapa nguvu maafisa wa kikoloni wa Ujerumani kuingia maeneo ya ndani kutwaa njia za biashara za wenyeji. Kufikia mwaka 1905, kampuni 200 zilifanya kazi zao Afrika Magharibi, 30 kati yake zilimilikiwa na Woermann peke yake. Zilikuwa zimeanzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama vile mafuta ya chikichi, kakao, tumbaku na kahawa nchini Kameruni, mbali sana kutoka bandarini.

 

Je, Mkataba wa Ujerumani na Douala haukukataza hili?

Wafalme wa Douala waliamini kwamba walichokuwa wamesaini yalikuwa makubaliano yanayoiruhusu Ujerumani kufanya shughuli zake kwenye eneo la mwambao tu. Lakini maafisa wa kikoloni waliwasilisha kwa wafalme hao waraka wa Kijerumani ambao ulikuwa umeshasainiwa. Kwa ardhi kuitwa mahamiya maana yake ni kuwa kampuni za Kijerumani zimeruhusiwa kufanya shughuli zake kwa msaada wa jeshi. Kupitia ulaghai huo, kidogo kidogo watu wa Douala wakaanza kupoteza udhibiti wa njia za biashara na ardhi zao za asili.


Vipi ukoloni uliwaathiri Wakameruni?

Bidhaa zilizosafirishwa ziliipatia Kampuni ya Woermann faida kubwa huku zikiharibu mfumo wa jamii ya Kameruni. Wengi wao hawakuwa wamewahi hata kuyasikia, seuze kukubaliana na masharti ya Mkataba wa Ujerumani na Douala. 

Maelfu ya wanaume na wanawake walilazimishwa kufanya kazi kwenye mashamba mapya, ambako hali ilikuwa mbaya na adhabu ya bakora ilikuwa ya kawaida.

Kivuli cha ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Kwanza

Maafisa katili wa kikoloni, kama Jesko von Puttkamer, walihakikisha kwamba Wakameruni kati ya 20,000 hadi 30,000 wanalazimishwa kuvuna na kusafirisha mpira kutoka maeneo ya ndani hadi kwenye meli zilizokuwa zikingoja bidhaa pwani. Viongozi wa kimila waliopinga hilo walidhalilishwa hadharani, vijiji viliteketezwa kwa moto, na hivyo kulazimisha watu wakimbilie kwenye miji iliyoanzishwa na Wajerumani.

Wakati Rudolf Douala Manga Bell, ambaye baba yake ndiye aliyesaini Mkataba wa Ujerumani na Douala mwaka 1884, alipolalamika kwamba watu wake walikuwa wananyanyaswa na ardhi yao inaporwa, alikamatwa kwa shutuma za uhaini na akanyongwa mwaka 1914.

Vipi Kampuni ya Woermann iliiathiri Namibia?

Kampuni ya Meli ya Woermann ilihodhi usafirishaji wa wanajeshi wa Kijerumani wapatao 15,000 kwenda Afrika Kusini Magharibi kuliangamiza Vuguvugu la Herero na Nama kati ya mwaka 1904 na 1907. Kampuni hiyo ilipata faida ya mamilioni ya fedha kwa kusafirisha maafisa hao wa kijeshi, bidhaa na vifaa kwa ajili ya serikali ya Ujerumani. Wakati fulani, fedha hizo zilifikia zaidi ya Mark 600,000,000, kiwango kikubwa sana kwa wakati huo ambacho kilitokana na fedha za walipakodi wa Ujerumani.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Pili

Watu wa Nama na Herero walionusurika na kampeni hiyo ya kijeshi walipelekwa magerezani katika maeneo ya Swakopmund na Lüderitz, ambako kampuni za Kijerumani, kama za Woermann, ziliwatumia wafungwa hao wa kivita kama watumwa kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu kama vile njia za reli na bandari.

 

Nini kilitokea baada ya Ujerumani kupoteza makoloni yake mwaka 1919?

Uhusiano wa karibu kati ya Kampuni ya Woermann na serikali ya Ujerumani ulipotea baada ya Ujerumani kulazimishwa kuyaachia makoloni yake yote baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Zama za biashara ya kinyonyaji wa kikoloni ilimalizika, lakini madhara yaliyotokana na uroho na ukatili huo bado yameacha majeraha kwenye jamii za watu wa Kameruni na Namibia hadi leo.

Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani zinatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa mambo ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.

Woermann Company,Germany,Cameroon,West Africa,Hamburg,Shadows of German Colonialism