1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za Ugavana Mombasa, Kakamega kukamilika

26 Agosti 2022

Kampeni za ugavana mjini Mombasa, pwani ya Kenya na Kakamega, Magharibi mwa nchi hiyo zinafikia kikomo Ijumaa hii huku wagombea wakiwa mbioni kuuza sera zao kwa wananchi katika kipindi hiki cha lala salama.

https://p.dw.com/p/4G4oe
Kenia | Unruhen vor Bekanntgabe des Wahlergenisses in Nairobi
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Kura za ugavana wa Mombasa zinatarajiwa kufanyika tarehe 29 Agosti mwaka wa 2022 huku kampeni za mwisho zikiendelezwa na wagombea kuwarai wananchi kuwapigia kura katika sehemu mbali mbali za Mombasa, pwani ya Kenya.

Uchaguzi wa ugavana wa Mombasa uliahirishwa tarehe 9 Agosti kutokana na hitilafu kwenye karatasi za kupigia kura. Na tarehe 23 Agosti iliyotangazwa kuwa tarehe mpya ya uchaguzi huo pia haukufanyika. Tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, kupitia mwenyekiti wake, Wafula Chebukati, ilisema ililazimika kuahirisha uchaguzi huo tena kutokana na vitisho na kunyanyaswa kwa maafisa wa tume hiyo.

Hatimaye, Jumatatu hii ndio siku ya wakaazi wa Mombasa kufanya maamuzi ya kumchagua gavana wao mpya ikizingatiwa kuwa hapo jana waliweza kuapishwa magavana wa kaunti zengine 45 huku zikisalia Kaunti ya Mombasa na Kakamega.

Huku shughuli za kawaida zikirejelewa katika Kaunti ya Mombasa, wananchi wanajiandaa kwenye kinyang'anyiro hicho cha ugavana huku wakitoa mwito wa amani kwa viongozi na raia kwa ujumla wakati wa zoezi hilo:

Maafisa wa IEBC wanasema wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha uchaguzi huo wa ugavana utafanyika kama ulivyopangwa. Kutakuwa na kinyang'anyiro kikali kwenye kura za ugavana miongoni mwa wagombea Hassan Omar Sarai wa chama cha UDA ambaye aliwahi kuhudumu kama seneta wa Kaunti ya Mombasa na Abdul-Swamad Nassir wa chama ODM ambaye amehudumu kama mbunge wa eneo bunge la Mvita. Nani ataibuka mshindi kati yao, ni jambo la kungoja na kuona.