1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi mkuu zaanza Uingereza

Admin.WagnerD6 Novemba 2019

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amemlinganisha mpinzani wake mkuu na muimla wa Usovieti Joseph Stalin huku akijiandaa kufungua rasmi kampeni za chama chake cha kihafidhina kwa uchaguzi wa  Disemba 12 inayokuja.

https://p.dw.com/p/3SZww
UK Wahlkampf Labour Partei
Picha: picture-alliance/ZUMA WIre/London News Pictures/R. Pinney

Katika wakati ambapo kampeni ambazo si rasmi zimeshaanza kuhanikiza tangu wiki kadhaa zilizopita, kampeni rasmi ya wiki tano imeanza leo baada ya bunge kuvunjwa.

Boris Johnson alikwenda katika kasri la Buckingham kumuarifu Malkia Elizabeth wa pili kabla ya kutoa hotuba  iliyofungua kampeni ya chama chake cha Kihafidhina.

Akisimama mbele ya ofisi na makaazi yake  huko Downing Street nambari 10, Boris Johnson amesema asingetaka uchaguzi wa mapema na hakuna yeyote anaetaka uchaguzi wa Desemba,lakini hawakuwa na njia nyengine.

Amewalaumu wabunge akisema "wamekataa kata kata kuidhinisha mchakato wa Brexit na kwa namna hiyo kuheshimu matokeo ya kura ya maoni.

Johnson ataka wapiga kura kupigia kura Conservatives

Großbritannien Brexit Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson Picha: imago images/PA Images/M. Crossick

Johnson amewatolea wito wapiga kura wakiunge mkono chama chake katika juhudi zake za kuitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kuambatana na makubaliano  aliyoyafikia pamoja na umoja huo.

Kampeni za uchaguzi zinaonyesha kuanza vibaya baada ya Boris Johnson kukituhumu chama kikuu cha upinzani kubuni mpango wa kupandisha kodi kwa kiwango cha juu kupita kiasi kwa namna ambayo zitavuruga mafanikio ya Uingereza.

Katika ripoti aliyoiandikia gazeti la Daily Telegraph, Johnson anakituhumu chama  hicho kinachofuata siasa ya kati kushoto kudhamiria kwa nguvu kuwasumbua matajiri kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu Stalin alipowaadhibu wakulak, yaani wakulima matajiri waliosumbuliwa vibaya sana na utawala wa Usovieti katika miaka ya 30.

Corbyn akosoa sera za uchumi za Johnson

Jeremy Corbyn Brexit London Großbritannien
Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/dpa/V. Flores

Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn ameitaja mipango ya kiuchumi ya Johnson kuwa ni yenye kufuata ule utaratibu wa waziri mkuu wa zamani Margreth Thatcher, akimaanisha utaratibu wa soko huru, na nadharia ya kupunguza matumizi.

Maneno hayo makali yamefuatia matamshi makali yaliyotolewa na chama cha Boris Johnson kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza.

Mkuu wa kundi la chama cha kihafidhina katika bunge lililomaliza mhula wake, Jacob Rees-Mogg alilazimika kuomba radhi kutokana na matamshi aliyoyatoa jana akisema wahanga wa  janga la moto lililoiteketeza nyumba moja ya mjini London na kuuwa watu 72 mwaka 2017 walikuwa wapumbavu walipoitika wito wa idara ya zima moto wa kusubiri msaada.