Kamerun yazindua kampeni ya kihistoria ya chanjo ya Malaria
23 Januari 2024Katika hospitali moja iliyoko mji wa Soa, takriban kilomita 20 kutoka mji mkuu Yaounde, mtoto kwa jina Noah Ngah mwenye umri wa miezi sita ndiye alikuwa wa kwanza kupata chanjo hiyo kwa jina RTS,S.
Chanjo hiyo ndiyo ya kwanza dhidi ya malaria ambayo imependekezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO.
Huku akishangiliwa na kutiwa moyo na wauguzi, mtoto huyo mchanga alipokea chanjo hiyo, jambo lilimfariji mama yake, ambaye alikuwa akisubiri dadake Noah ambaye ni pacha pia apate chanjo.
Mama huyo kwa jina Helene Akono ameliambia shirika la habari la AFP kwamba baadhi ya wazazi wamenyamaza lakini anajua kuwa chanjo hiyo ni nzuri kwa watoto.
Kulingana na shirika la Afya Duniani WHO, ugonjwa wa Malaria unaosababishwa na mbu huua zaidi ya watu 600,000 kila mwaka hasa barani Afrika.
Asilimia 80 ya vifo hivyo barani Afrika ni vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
Kufuatia awamu ya majaribio, chanjo ya RTS,S inasambazwa kwa kiwango kikubwa barani Afrika, kuanzia Cameroon.
Akishangiliwa na kutiwa moyo na wauguzi, mtoto huyo mchanga alipokea chanjo hiyo -- kiasi cha kumfariji mama yake, ambaye alikuwa akisubiri kuchanjwa pia dadake pacha.
Soma pia: Cape Verde yatangazwa kutokomeza ugonjwa wa Malaria
Hospitali hiyo ya mjini Soa, ni mojawapo ya vituo vingi vya chanjo katika wilaya 42 zilizopewa kipaumbele katika taifa hilo kubwa la Afrika ya kati lenye takriban watu milioni 28.
Kulingana na serikali ya Kameruni, chanjo hiyo itatolewa bila malipo na kwa watoto wote walio chini ya umri wa miezi sita. Itatolewa kwa wakati mmoja na chanjo nyingine za lazima au zinazopendekezwa.
Hatua ya kihistoria kwa Afrika
Mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, linalowahudumia watoto la UNICEF na muungano wa watengeneza chanjo Gavi, walisema hatua hiyo ni "ya kihistoria kuelekea chanjo pana dhidi ya ugonjwa hatari zaidi kwa watoto wa Afrika".
Zaidi ya dozi 300,000 za chanjo aina ya RTS,S ziliwasili Yaounde mwishoni mwa mwezi Novemba.
Ilichukua muda wa miezi miwili kuweka taratibu za uzinduzi wa chanjo hiyo siku ya Jumatatu.
Tangu mwaka 2019, zaidi ya watoto milioni mbili walipata chanjo hiyo nchini Ghana, Kenya na Malawi katika awamu ya majaribio.
Matokeo ya hatua hiyo yalionesha kupungua kwa ugonjwa wa malaria na vilevile upungufu wa wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa kiasi kikubwa.
Willis Akhwale, mshauri maalum katika Baraza la kutokomeza Malaria nchini Kenya End Malaria Kenya, alisema uzinduzi huo wa chanjo ni afueni lakini sio kile alichokitaja kuwa silaha pekee dhidi ya Malaria.
Soma pia: WHO kutanua utolewaji chanjo ya Malaria kwa watoto Afrika
Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "ufanisi wake, pamoja na kwamba unaokoa maisha, si kwa asilimia 100. Lakini hata kwa asilimia 40, unaokoa maisha na hasa katika umri wa miaka miwili unapoelekea kupata malaria kali.
Nchi ya kwanza duniani
Kulingana na shirika la WHO, ambalo ndilo linaratibu kampeni hiyo inayofadhiliwa na Gavi, Cameroon ndiyo nchi ya kwanza duniani ambako chanjo hiyo imeanza kutolewa kwa kiwango kikubwa na kwa utaratibu maalum.
Aurelia Nguyen, afisa mkuu wa mpango huo wa muungano wa Gavi, amesema nchini Cameroon, asilimia 30 ya mashauriano yalihusiana na malaria.
Amesema Kuwa na zana za kinga kuzuia kama chanjo, kutaweka huru mfumo wa afya na kupunguza idadi ya wanaolazwa hospitalini n ahata vifo kutokana na malaria.
Burkina Faso, Liberia, Niger na Sierra Leone pia zimepangwa kuzindua programu kubwa za chanjo dhidi ya Malaria baada ya Cameroon.