Kamati ya maadili ya wabunge wa CCM yawahoji wabunge watatu
3 Septemba 2021Kuhojiwa kwa wabunge Josephat Gwajima na Jerry Silaa kunafuatia agizo la bunge la Tanzania kuwapa adhabu ya kuwasimamisha wabunge hao kuhudhuria mikutano miwili ya bunge na kuiagiza kamati ya maadili ya wabunge wa CCM kuwahoji baada ya kukutwa na hatia ya kusema uongo na kushusha hadhi ya bunge.
Akizungumza mbele ya wandishi wa habari Katika ofisi za makao makuu ya CCM Jijini Dodoma mara baada ya kumaliza kwa mahojiano na wabunge hao, Mwenyekiti wa kamati ya maadili ya wabunge wa CCM Hassan Mtenga, amesema kuwa kamati yake imewahoji wabunge hao kufuatia agizo la bunge na kuongeza kuwa.
Aidha Mwenyekiti huyo wa kamati ya maadili ya wabunge wa chama cha mapinduzi CCM, ameweka hadharani sababu ya mbunge wa kuteuliwa wa chama hicho Amphrey Polepole, kuwa amefikishwa katika Kamati hiyo hasa kutokana na kauli zake mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa katika mitandao ya kijamii na hivyo kuzua taharuki miongoni mwa jamii.
Kamati Kuu ya CCM na hatma ya wabunge
Adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya bunge kwa wabunge Josephat Gwajima na Jerry Silaa ilotolewa hivi karibuni huku Kamati ya Kudumu ya haki, maadili na madaraka ya bunge ikikielekeza chama cha CCM kuwahoji wabunge hao kutokana tuhuma zinazowakabili.
Mbunge Askofu Josephat Gwajima alifikishwa mbele ya Kamati hizo kufuatia kauli zake kuhusiana na chanjo dhidi ya COVID-19 ambazo amekuwa akizitoa katika kanisa lake la ufufuo na uzima kuwa hazifai huku akiwahimiza waumini wa kanisa lake ulimwenguni kote ikiwemo Tanzania kutokuchanja hadi pale serikali itakapotoa ufafanuzi wa kutosha kuhusiana na usalama wa chanjo hiyo wakati mbunge wa Ukonga Jeryy Silaa akikutwa kosa la kusema uongo ikiwemo kauli yake ya kuwa Wabunge wa Tanzania hawalipi kodi hivyo wanapaswa kulipa kodi kama wafanyavyo wananchi wengine.