Kamati kuu ya ANC kuamua hatma ya Ramaphosa Afrika Kusini
5 Desemba 2022Viongozi wa ngazi za juu ndani ya chama tawala nchini Afrika Kusini ANC wako kwenye mazungumzo yaliyoanza Jumatatu kujadili hatma ya rais Cyril Ramaphosa madarakani. Kikao cha ANC kinafanyika wakati Jumanne bunge linatarajiwa kupiga kura katika hatua ambayo inaweza kumuondowa madarakani. Mkutano huo utatowa maamuzi ikiwa Ramaphosa anabakia kuwa mwenyekiti wake au anapaswa kuondolewa.
Mwishoni mwa juma rais Ramaphosa alisisitiza kwamba hatojiuzulu baada ya jopo maalum kutoa ripoti yake kuhusu tuhuma za kumuhusisha kiongozi huyo na kadhia ya kuficha tukio wizi wa fedha uliotokea baada ya makaazi yake ya shambani kuvamiwa na kuvunjwa na majambazi. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kwamba mustakabali wa kisiasa wa rais huyo bado haujulikani.
Siku ya Jumatatu Ramaphosa alionekana akiwasili kwenye eneo la mkutano wa kamati kuu ya chama cha ANC,NEC ambayo ndio chombo chenye maamuzi ya mwisho ya chama,lakini aliondoka muda mfupi baadae akionekana mwenye kutabasamu na kuwapungia mkono waandishi habari.
Msemaji wa ANC Pule Mabe alisema rais amezuiwa kuingia kwenye mkutano kwa mujibu wa utaratibu uliopo,kwasababu mjadala unaofanyika unamuhusu yeye.
Mkutano huo kwa mujibu wa Mabe unalenga kupata mtazamo wa busara wa pamoja
Chama cha ANC kilichoanzishwa na Nelson Mandela kama silaha iliyoongoza mapmbano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kimeingia kwenye mpasuko mkubwa kikigawika kutokana na masuala yake ya ndani ingawa baada ya vuta ni kuvute wengi sasa ndani ya chama hicho wanaonesha kumuunga mkono rais huyo.
Na kwakuwa Jumatatu ni maadhimisho ya miaka tisa tangu alipofariki Mandela msemaji wa chama Mabe amesema katika kumkumbuka kiongozi huyo chama hicho kitahakikisha kinaumaliza mkutano wake kwa kuonesha mshikamano.Hata hivyo miito imekuwa ikisikika miongoni mwa wananchi wa Afrika Kusini wakikitaka chama hicho kimshinikize Ramaphosa ajiuzulu.
Siku ya Jumanne ripoti ya uchunguzi iliyomuweka mashakani Ramaphosa itajadiliwa bungeni hatua ambayo inaweza kupelekea kuitishwa mchakato wa kupigwa kura itakayoamua hatma ya Ramaphosa madarakani.
Ingawa ili alazimike kuondoka madarakani patahitajika thuluthi mbili ya wabunge watakaounga mkono hatua hiyo.Japo ikumbukwe pia chama cha ANC kinashikilia viti 230 katika bunge la viti 400.