Kamanda wa zamani wa LRA atiwa hatiani kwa uhalifu Uganda
14 Agosti 2024Uamuzi uliosubiriwa kwa muda mrefu katika kesi ya Thomas Kwoyelo ulitolewa Jumanne na jopo la Mahakama Kuu lililoketi Gulu, mji wa kaskazini ambapo LRA ilikuwa inaendesha uasi wake. Ilikuwa ni kesi ya kwanza ya ukatili kuhukumiwa chini ya kitengo maalum cha Mahakama Kuu ambacho kinaangazia uhalifu wa kimataifa.
Kwoyelo alikabiliwa na mashtaka yakiwemo mauaji, wizi, utumwa, vifungo, ubakaji na ukatili. Alipatikana na hatia katika makosa 44 kati ya 78 aliyokabiliwa nayo kwa uhalifu alioutenda kati ya 1992 na 2005. Haijabainika mara moja atahukumiwa lini.
Kwoyelo, ambaye kesi yake ilianza kusikilizwa mwaka wa 2019, alikuwa kizuizini tangu 2009 huku mamlaka ya Uganda ikijaribu kutafuta jinsi ya kutoa haki kwa njia ya usawa na ya kuaminika. Human Rights Watch iliielezea kesi yake kama "fursa adimu ya haki kwa waathirika wa vita vya miongo miwili kati ya" wanajeshi wa Uganda na kundi la LRA.
Soma pia: ICC yaongeza juhudi za kufufua kesi dhidi ya Joseph Kony
Waendesha mashtaka walisema Kwoyelo alikuwa na cheo cha kijeshi cha kanali ndani ya LRA na kwamba aliamuru mashambulizi ya kikatili dhidi ya raia, wengi wao wakiwa wale waliokimbia makazi yao kutokana na uasi huo.
Kiongozi wmkuu wa LRA, Joseph Kony, anaaminika kujificha katika eneo kubwa la msitu usio na udhibiti Afrika ya kati. Marekani imetoa dola milioni 5 kama zawadi kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa Kony, ambaye pia anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.
Mmoja wa makamanda wa Kony, Dominic Ongwen, alihukumiwa mwaka 2021 na ICC kifungo cha miaka 25 jela kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Uendeshaji wa kesi hiyo
Kwa ujumla Kwoyelo alipatikana na hatia katika makosa 44 kati ya 78 yaliyokuwa yakimkabili kutokana na uhalifu alioutenda kati ya mwaka 1992 na 2005 hasa katika eneo anakotoka la Amuru kaskazini mwa Uganda na maeneo kadhaa ya Sudan Kusini.
Hata hivyo haijabainika wazi ni lini atahukumiwa rasmi. Naibu mwendesha mashtaka wa umma William Byansi aliiomba mahakama ipewe muda wa kutafuta kile kilichoitwa "hukumu inayofaa zaidi" kwa Kwoyelo. Lakini mmoja wa mawakili wa Kwoyelo, Caleb Alaka, amesema mahakama inapaswa kuzingatia mambo mengine ikiwamo kukaa kwake rumande kwa muda mrefu.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwaka 2019 na alikuwa kizuizini tangu 2009 huku mamlaka ya Uganda ikijaribu namna ya kutekeleza haki kwa njia ya usawa na ya kuaminika. Kwoyelo, ambaye alitekwa nyara na LRA akiwa na umri wa miaka 12 na kuwa kamanda wa ngazi ya chini, hapo awali alikana mashtaka yote dhidi yake.
Maelfu ya wapiganaji wengine waasi wamepokea msamaha wa serikali ya Uganda kwa miaka mingi, lakini Kwoyelo, ambaye alikamatwa katika nchi jirani ya Kongo, alinyimwa msamaha huo. Maafisa wa Uganda hawajawahi kueleza kwa nini.
Kulikuwa na wasiwasi wa wanaharakati wa haki kwamba kuchelewesha kesi yake kwa muda mrefu kulikiuka haki zake za msingi.
Soma pia:Lord's Resistance Army (LRA)
Kesi yake iligubikwa na utata, na kutilia mkazo juu ya changamoto zan utoaji haki katika jamii ambayo bado inatibu vidonda vya vita. Kama ilivyokuwa katika kesi ya Ongwen katika mahakama ya ICC, Kwoyelo alidai kwamba alitekwa nyara akiwa mvulana mdogo ili kujiunga na safu ya LRA na kwamba hangeweza kuwajibika kwa uhalifu wa kundi hilo.
"Kony ndiye anapaswa kushtakiwa kila kosa"
Kwoyelo, ambaye alikanusha mashtaka dhidi yake, alitoa ushahidi kwamba ni Kony pekee ndiye angeweza kujibu uhalifu wa LRA, na kusema kila mtu katika LRA alikabiliwa na kifo kwa kutomtii mbabe huyo wa vita.
Kundi la LRA, ambalo lilianza nchini Uganda kama uasi dhidi ya serikali, lilishutumiwa kwa kuwaandikisha wavulana kupigana na kuwatumia wasichana kama watumwa wa ngono.
Soma pia: ICC kutoa uamuzi rufaa ya mbabe wa kivita wa kundi la LRA
Katika kilele cha nguvu yake, kundi hilo lilifanya ukatili wa kupindukia, ambalo wanachama wake kwa miaka walivikwepa vikosi vya Uganda kaskazini mwa Uganda. Uasi wake dhidi ya utawala wa Rais Yoweri Museveni ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 100,000, na watoto 60,000 kutekwa nyara.
Baadhi ya waangalizi wameeleza kuwa makamanda wa kijeshi wa Uganda waliotajwa katika unyanyasaji wa raia wakati wa uasi wa LRA hawajakabiliwa na mkono wa sheria.
Kundi la LRA lilishutumiwa kufanya mauaji mengi yanayolenga zaidi watu wa kabila la Acholi. Joseph Kony, ambaye pia ni Mwacholi, alijitangaza kuwa masihi ambaye alisema mapema katika uasi wake kwamba alitaka kuitawala Uganda kulingana na Amri Kumi za Biblia.
Wakati shinikizo la kijeshi lilipolazimisha LRA kuondoka Uganda mwaka 2005, waasi wake walitawanyika katika maeneo ya Afrika ya kati. Kundi hilo limefifia katika miaka ya hivi karibuni, na ripoti za mashambulizi ya LRA ni nadra.
Chanzo: APE