Kaka wawili Boateng kukabana koo
20 Septemba 2013Bayern wanacheza ugenini, nyumbani kwa Schalke, Veltins Arena kupambana na timu hiyo ya Gelsenkirchen inayoonekana kujiimarisha kwa kushinda mechi zake nne za mwisho baada ya mwanzo mbaya.
Tangu kuwasili kwake akitokea AC Milan mwezi uliopita, Kevin Prince Boateng amesaidia kuinyanyua Schalke hadi nafasi ya tisa huku mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ghana akiongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Kevin Prince Boateng aongeza nguvu Schalke
Prince Boateng mwenye umri wa Smiaka 26 alifunga bao la ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Mainz mwishoni mwa wiki iliyopita na akafunga goli la pili katika ushindi wao wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Steaua Bucharest katika Champions League siku ya Jumatano.
Mabingwa Ulaya Bayern watakuwa kipimo kikubwa kwa mfululizo wa ushindi wa Schalke, lakini cha kuvutia katika mechi hiyo ni wakati kaka wa Boateng watakapokutana ana kwa ana. Kevin Prince Boateng mzaliwa wa Berlin anasema hakutakuwa na mapenzi uwanjani kati yake na kaka Jerome Boateng. Bayern wameangusha pointi mbili pekee kutokana na mechi zao tano za kwanza za Bundesliga na wameanza kampeni yao ya kuhifadhi taji la Champions League kwa ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya CSKA Moscow. Jerome Boateng mwenye umri wa miaka 25 anasema anataraji kutoka Gelsenkirchen na pointi tatu zaidi za ligi, na hatajaribu kumbembeleza kakake uwanjani. Anasema atajaribu kutomwangusha chini, lakini kama hapatakuwa an mbinu nyingine, basi atafanya hivyo. Mara ya mwisho kaka hao wawili kukutana ilikuwa mwaka wa 2010 wakati wa Dimba la Dunia nchini Afrika Kusini ambapo Ujerumani iliishinda Ghana bao moja kwa sifuri.
Bayern watakosa huduma za Javi Martinez, wakati pia Mario Götze akiwa nje, ijapokuwa kiungo Bastian Schweinsteiger huenda akashirikishwa. Schalke nao bado hawana huduma za mshambuliaji Mholanzi Klaas-Jan Huntelaar. Katika mechi zitakazochezwa kesho Jumapili, Freiburg v Hertha Berlin, VfB Stuttgart v Eintracht Frankfurt
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu