1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za mashirika mbalimbali ya Kijerumani dhidi ya chuki dhidi ya Wageni

Peter Philipp / Maja Dreyer28 Agosti 2007

Hivi punde tuliripoti juu ya Wahindi kadhaa walioshambuliwa na vijana Manazi katika mjini mdogo jimboni Saxony, Ujerumani. Tangu hapo, nchini humu kunaendelea mjadala juu ya mikakati ya kupambana na makundi yenye misimamo mkali ya kisiasa na kupinga wageni.

https://p.dw.com/p/CHjX
"Tatizo ni ubaguzi wa kimbari"
"Tatizo ni ubaguzi wa kimbari"Picha: picture-alliance/ dpa

Mashirika mbali mbali, yawe ya kiserikali au yasiyo ya kiserikali, ya kanisa au ya watu binafsi yanayoshughulikia kuwamotisha wananchi dhidi ya sera kali. Mwandishi wetu Peter Philipp anatambulisha mawili kati yao na kazi zao nzuri kuhusu suala hili. Msimulizi wake ni Maja Dreyer.

Hakuna takwimu kuhusu idadi ya mashirika yanayojitolea kupambana na sera kali za mrengo wa kushoto, makundi ya Manazi na chuki dhidi ya wageni. Mjini Cologne pekee, zaidi ya makundi 12 yaliungana katika jumuiya yakiwemo makundi yenye umaarufu kutokana na kuungwa mkono na wanasiasa maarufu, mengine hayajulikani sana. Pengine ni ushirikiano miongoni mwa wakaazi wa mtaa fulani au ni juhudi za polisi kuwafahamisha wanafunzi wa shule vipi wanaweza kujikinga na mashambulizi.

Mfano wa kwanza ambao uzingatiwe kwa kina ni jumuiya ya familia zilizo na asili ya nchi mbili. Meggie Kleine-Salgar wa jumuiya hiyo anaendesha mradi kwenye shule za chekechea mjini Bonn. Kwani tayari katika shule hizo kuna watoto wa asili mbali mbali wanaoongea lugha tofauti, wazazi wao wakiwa wa madhehebu tofauti na tamaduni mbalimbali. Kwa hivyo, ni vigumu kwa walimu wa watoto hao wadogo kutafuta njia mwafaka ya kuwaelimisha wote, anaeleza Bi Kleine-Salgar: “Ni jambo la kawaida kuwa na mchanganyiko wa watoto wa asili mbali mbali, lakini walimu hawakupewa mafunzo yapasavyo. Wana shinda kubwa na kwa hivyo wanahitaji msaada.”

Kwa mujibu wa Bi Kleine-Salgar ni muhimu sana kuwa kuanzia mwanzo watoto wanafundishwa vizuri juu ya jamii inayounganisha watu wa asili mbali mbali ili kuzuia kuwepo hisia au chuki dhidi ya watu wa asili tofauti. Pale walimu wa shule za chekechea wanaposhindwa, matatizo yatakuwa makubwa zaidi wakati watoto wanaanza shule.

Walimu wanapokea vizuri msaada kutoka nje na wanataka kutafuta suluhisho, anasema Meggie Kleine-Salgar. Lakini kwa upande wa wazazi kuna upinzani: “Kuna wazazi fulani ambao wanataka watoto wao waende kwenye shule yenye watoto wa Kijerumani tu wanaoongea Kijerumani tu. Hawatambui kuwa ni lazima kujihusisha na tamaduni nyingine, hata wakiwa ni wazazi tu.”

Shirika lingine tunalolitambulisha kidogo ni wakfu wa vyombo vya habari vya Civis ambao una mkakati mwingine tofauti kabisa. Kila mwaka, wakfu hiyo inatoa tuzo kwa vipindi vilivyorushwa kwa vyombo vya habari vya Umoja wa Ulaya ambavyo vinaelemisha vizuri na kwa njia ya kisasa namna ya kuwajumuisha wageni katika jamii.

Lengo la kutoa tuzo hilo si tu kuwafahamisha watangazaji na wasikilizaji, bali pia ni kuwapa motisha waandishi wa habari walishughulikie suala hilo na chuki dhidi ya wageni. Tangu mada hiyo kupewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari, wananchi wanavutiwa zaidi na masuala haya, anasema Bw. Michael Radix, mkuu wa wakfu huu: “Bila shaka suala la kuwaunganisha wageni katika jamii na kuwepo kwa tamaduni mbali mbali limezidi kupata umuhimu kwenye jamii yetu. Pengine hata ni kazi yetu kuu katika siku za usoni kuwezesha maisha ya pamoja na ya amani katika jamii za Ulaya zinazounganishwa na wahamiaji.”