1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Makundi ya Upinzani Riyadh

8 Desemba 2015

Mkutano wa makundi ya upande wa upinzani ya Syria utaitishwa Saudi Arabia katika wakati ambapo nchi shirika zinazoongozwa na Marekani zinakabiliwa na kishindo baada ya mabomu yao kuwauwa raia wasiopungua 36.

https://p.dw.com/p/1HJ6q
Mfalme Salman Ibn Abdulaziz wa Saud ArabiaPicha: picture-alliance/dpa/O. Douliery

Mkutano wa makundi ya upande wa upinzani ya Syria unapangwa kuitishwa nchini Saudi Arabia. Mkutano huo unaitishwa katika wakati ambapo nchi shirika zinazoongozwa na Marekani zinakabiliwa na kishindo kikubwa baada ya ndege zao za kijeshi kuvurumisha mabomu na kuwauwa raia wasiopungua 36.

Saudi Arabia ilitangaza mwezi uliopita,itaitisha mkutano kwa lengo la kuyaleta pamoja makundi ya kisiasa na kijeshi ili kuunda muungano utakaoshiriki katika mazungumzo ya siku za mbele pamoja na serikali ya rais Bashar al Assad wa Syria.

Kundi la waasi la "Jaish al Islam ( au jeshi la kiislam),linalotajikana kujivunia uungaji mkono wa Saudi Arabia, limeshasema litashiriki katika mazungumzo hayo ya Ryadh. Katika risala yao kupitia mtandao,msemaji wa Jaesh al Islam,amesema watawakilishwa na watu wawili,Mohammed Alloushe na Mohammad Birqdar katika mkutano huo uliopangwa kuanza jumatano.

Jaish al Islam linatajikana kuwa kundi kubwa zaidi la waasi wanaokutikana karibu na mji mkuu wa Syria Damascus, wakidhibiti sehemu kubwa ya kitongoji cha mji mkuu-Ghouta,kitovu cha mashambulio ya mara kwa mara ya vikosi vya serikali. Kundi jengine la waasi wanaokutikana zaidi katika maeneo ya kusini mwa Syria nao pia wamealikwa kuhudhuria mazungumzo hayo ya Riyadh,sawa na Ahrar al Cham. Waliotengwa ni pamoja na wanamgambo wa dola la kiislam IS na tawi la Al Qaida nchini Syria-Al Nusra sawa na makundi ya wakurd na vikosi huru vya Syria,ambao ni muungano wa wanamgambo wa kikurd,kiarabu na kikristo.

Wapinzani zaidi waachiliwa huru Homs

Wakati huo huo serikali ya Syria imewaachia huru wafungwa wa upande wa upinzani katika mji wa kati ya Homs,hiyo ikiangaliwa kama ishara ya nia njema kabla ya makubaliano yatakayopelekea kuondoka maelfu ya wapiganaji wa upande wa upinzani kutoka mji huo . Gavana wa Homs,Talal Barrazi amesema hii ni mara ya tano kwa wafungwa wa upinzani kuachiwa huru,akiahidi na wengine zaidi watafuatia. Itafaa kusema hapa kwamba wakaazi wa mji huo walikuwa wa mwanzo kuteremka majiani mwaka 2011 kulalamika dhidi ya utawala wa rais Bashar al Assad.

Syrien Bürgerkrieg ausländische Kämpfer bei der kurdischen YPG
Wapiganaji wa kigeni miongoni mwa wanamgambo wa kikurd-Peshmerga nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/U. Onder Simsek

Hujuma za ndege za nchi shirika zinazoongozwa na Marekani

Na raia wasiopungua 36 wameuwawa ndege za kivita zinazoongozwa na Marekani zilipotupa mabomu katika kijiji cha Al Khan kaskazini mashariki ya Syria. Hujuma hizo ni za pili katika kipindi cha siku moja tu, baada ya zile zilizopelekea kuuliwa wanajeshi wasiopungua watatu wa Syria jumapili iliyopita.

Ali Akbar Velayati und Bashar Assad in Syrien
Rais Bashar Al Assad (kulia)akizungumza na mshauri wa ngazi ya juu wa kiongozi wa kidini wa Iran,Ayatollah Ali Khamenei,Ali Akbar VelayatiPicha: picture-alliance/dpa/SANA

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri:Yusuf Saumu