1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuleta amani Syria

5 Novemba 2013

Mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria Lakhdar Brahimi, anakutana na maafisa wa Urusi na Marekani mjini Geneva. katika wakati ambapo Umoja wa mataifa unasema asili mia 40 ya wa Syria wanahitaji kusaidiwa.

https://p.dw.com/p/1ABgZ
Bibi mkimbizi huyo akimpakata mwanawe karibu na hema katika kambi ya wakimbizi ya Bekaa,mashariki ya LibnanPicha: Reuters

Tuanzie na hali mbaya inayowasumbua wakaazi wa Syria.Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa watu milioni tisa na laki tatu,kiwango ambacho ni sawa na asili mia 40 ya wakaazi jumla wa nchi hiyo wanahitajai msaada wa kiutu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa."Hali inazidi kuwa mbaya" amesema msemaji wa naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anaeshughulikia masuala ya kiutu,Valerie Amos,Amanda Pitt.

Wakati huo huo juhudi za kimataifa za kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Syria zinashika kasi.Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi yuko Geneva kwa mazungumzo pamoja na manaibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Mikhail Bogdanov na Guennady Gatilov na mwenzao wa Marekani anaeshughulikia masuala ya kisiasa Wendy Sherman.

Lakhdar Brahimi
Mpatanishi wa kimataifa Lakhdar BrahimiPicha: Reuters/Khaled al-Hariri

Mkutano huo utafuatiwa na kikao chengine kitakachohudhuriwa pia na wawakilishi wa mataifa mengine matatu yenye kura ya turufu katika baraza la usalama la umoja wa Mataifa,China,Ufaransa na Uingereza.

Kuendelea kuwepo madarakani rais Bashar al Assad katika kipindi cha mpito ni miongoni mwa pingamizi kadhaa za mkutano wa Geneva.Upande wa upinzani unadai upatiwe hakikisho kwamba mkutano huu utapelekea kung'oka madarakani utawala wa Bashar al Assad.Jana usiku lakini waziri wa habari wa Syria,Omrane al Zohbi alisema utawala wa rais Bashar al Assad haufikirii kwenda Geneva kwa lengo la "kukabidhi madaraka".

John Kerry
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Getty Images/Mark Wilson

Marekani haitoingilia kijeshi

Wawakilishi wa upande wa upinzani wanakutana jumamosi ijayo mjini Istanbul kuamua kama washiriki katika mkutano wa Geneva au la.Baraza la taifa la Syria-kundi kubwa kabisa miongoni mwa makundi yanayounda muungano wa upande wa upinzani,limeshasema halitoshiriki katika mazungumzo hayo na limefika hadi ya kutishia kujitenga na muungano huo pindi ukiamua kushiriki.

Akiwa ziarani nchini Saud Arabia,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema kwa mara nyengine tena Washington haitoingilia kijeshi nchini Syria.Amehakikisha nchi yake inaunga mkono msimamo wa nchi za kiarabu wa "kuiokoa Syria na kuundwa serikali ya mpito" itakayowapatia fursa wananchi wa Syria waamue kuhusu mustakbal wao.

Mwandishi: Hamidou/Reuters/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef