Chama tawala Tanzania champata mgombea wa urais
12 Julai 2015Waziri Magufuli mwenye umri wa miaka 55 anatarajiwa kuchukuwa nafasi ya Rais wa sasa Jakaya Kikwete pindi CCM kitashinda uchaguzi huo. Kwa mujibu wa matokeo, Magufuli alipata asilimia 87 ya kura akifuatiwa na balozi Amina Salim Ali asilimia 10 na Dr Asha Migiro asilimia 3. Magufuli hakuwa akitajwa kuwa mgombea wa usoni miongoni 38 waliojitokeza wakiwemo makamu wa Rais Mohammed Gharib Bilal, Waziri mkuu Mizengo Pinda na Mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye. Hata hivyo alifanikiwa hatimae kuwa kwenye orodha ya wagombea watatu wa mwisho.
Tanzania ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 45, ni taifa la Afrika mashariki lenye ukuaji uchumi wa zaidi ya asilimia 7-ikiwa ni kwa mujibu wa Benki ya dunia. Licha ya maendeleo hayo, taifa hilo linasalia kuwa masikini sana katika ukanda huo wa Afrika mashariki na hata katika viwango vya kimataifa, huku Benki ya dunia ikisema sekta muhimu ya kilimo ikitoa robo moja tu ya ya pato jumla la taifa . Robo tatu ya wakaazi wake wanajishughulisha na kilimo kuweza kuishi.Chama tawala CCM kimekumbwa na tuhuma za rushwa na upendeleo, jambo moja wapo lililotawala katika mchakato wa kumpata mgombea wake.
Mchakato huo wa kumpata mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao, umemalizika leo alasiri kwa mkutano mkuu kumuidhinisha pia Dr Ali Mohamed Shein kuwa mgombea Urais huko Zanzibar kwa mara nyengine Baada ya kumpitisha awali 2010. Pia Mgombea Urais wa Muungano Waziri Magufuli alimtangaza mgombea wake mwenza ambaye ni Bibi Samia Suluhu Hassan.
Pindi CCM ikishinda mwezi Oktoba, atakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya taifa hilo kushika wadhifa huo wa pili katika ngazi ya uongozi na Tanzania kufuata nchi nyengine mbili za ukanda huo ambazo zimewahi kuwa na makamu wa rais wanawake-nazo ni Uganda na Burundi.
Wakati huo huo, wanasiasa wa upinzani wameanza mchakato wa kuwatafuta wagombea wao wa urais. Kwa upande mwengine muungano unaojulikana kama Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA ukiendelea na mazungumzo ya kuwa na mgombea mmoja wa urais. Pia umekuwa ukisema kwamba vyama vinavyounda muungano huo- Chadema, CUF,NCCRMageuzi na NLD, vimekubaliana kuwa wagombea wa pamoja kwenye majimbo. Kuna wanaoamini kwamba upinzani safari hii utaweza kufanya vizuri zaidi ikiwa utaungana .
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohamed Dahman