1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 33 wauwawa baada ya sumu ya gesi kudondoshwa Saraqeb

Mjahida2 Agosti 2016

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameihimiza Urusi na serikali ya Syria kujizuwiya kushambulia wakati mapigano yakiendelea siku ambayo alitumai kipindi cha mpito cha kisiasa kitaanza.

https://p.dw.com/p/1JaBD
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/J. Roberts

"Ni muhimu kwamba Urusi ijizuwiye kushambulia pamoja na utawala wa rais Assad, kama ilivyo wajibu wetu wa kutaka upinzani pia kujizuwiya kushiriki katika mashambulio," alisema Waziri Kerry alipozungumza na waandishi habari mjini Washington.

Ameongeza kuwa mashambulio kutoka serikali ya Assad yamezuwiya pande zinazohasimiana kukutana kwa majadilianpo hapo jana Jumatatu siku ambayo ililengwa kwa maafisa wa upinzani na serikali kukubaliana juu ya namna ya kutekeleza kipindi cha mpito cha kisiasa.

Kerry amesema upinzani haukuona sababu ya kukutana mjini Geneva kwa mazungumzo wakati mapigano yakiwa bado yanaendelea. Vikosi vya rais Bashar al Assad vimezingira maeneo yanayoshikiliwa na waasi mjini Aleppo moja ya mji uliyoathirika zaidi na mapigano tangu yalipoanza mwaka wa 2011.

Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: picture alliance/AP Photo

Mji huo umekumbwa na mapigano makali katika siku za hivi karibuni hii ikiwa ni hatua ya waasi kujaribu kusitisha mzingiro wa serikali katika eneo hilo na kukata barabara inayotumiwa na serikali kuingia Kaskazini mwa mji huo.

Aidha Urusi na Marekani wamekuwa msitari wa mbele katika juhudi za Kimataifa za kujaribu kuuleta utawala wa Rais Assad kwenye mazungumzo na makundi ya waasi waliyojihami.

Gesi ya sumu yatumika mjini Saraqeb wanawake na watoto waathirika zaidi

Huku hayo yakiarifiwa kundi la huduma za uokozi linalofanya kazi katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi limesema helikopta moja imedondosha makonteina ya gesi iliyo na sumu usiku mzima, katika mji mmoja karibu na mahala helikopta ya Urusi ilipodunguliwa hapo jana.

Aleppo Syrien Senfgas Anschlag IS Daesh
Mtu aliyeathirika na gesi ya sumu apata matibabu SyriaPicha: picture-alliance/AA/M.Omer

Msemaji wa ulinzi wa raia nchini Syria ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu 33 wengi wao wanawake na watoto wameathirika na gesi hiyo ya sumu mjini Saraqeb.

Kundi hilo la uokozii lilituma mkanda wa video katika mtandao wa kijamii wa You Tube ukionyesha idadi kadhaa ya wanaume wakijaribu kupumua na wakisaidiwa kwa kupewa vifaa vya kuwasaidia kupumua na watu waliyovalia sare za kundi la ulinzi wa raia.

Hata hivyo serikali na upinzani wameendelea kukanusha kutumia gesi ya sumu katika mapigano yanayoendelea kwa miaka mitano sasa. Serikali za Magharibi zimekuwa zikiilaumu serikali ya Syria kutumia gesi aina ya Chlorine dhidi ya raia wake. Huku serikali na mshirika wake Urusi wakiulaumu upinzani kutumia gesi ya sumu katika mapigano hayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo