JOHANNESBERG: Mwanamke wa Uingereza akamatwa kwa kufanya ujasusi Angola
20 Februari 2007Mwanamke mmoja raia wa Uingereza, Sarah Wykes, anayefanya kazi na shirika la kutetea haki za binadamu la Global Witness, lenye makao yake mjini London, amekamatwa na kushtakiwa kwa kufanya ukachero nchini Angola.
Shirika la Global Witness limesema mwanaharakati huyo aliyekuwa nchini Angola kukutana na wajumbe wa mashirika ya kiraia, alitiwa mabaroni na polisi juzi Jumapili asubuhi katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Cabinda.
Mmoja wa mawakili wa Sarah Wykes, Martin Nombo, amesema mteja wao alifikishwa mahakamani jana baada ya kulala gerezani. Aidha Nombo alisema yeye na mawakili wengine wawili walifukuzwa nje ya mahakama wakati mama huyo alipowasili katika mahakama hiyo.
Gereza anakozuiliwa mwanamke huyo imeelezwa kuwa katika hali mbaya huku kukiwa na uchafu, ukosefu wa hewa safi na maji.