1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jitihada mpya za kusitisha mapigano Syria

22 Septemba 2016

Tofauti kati ya Marekani na Urusi kuhusiana na mzozo nchini Syria zimefikia kiwango kipya baada ya mataifa hayo mawili kushtumiana vikali kwa madai ya unafiki na ufisadi katika Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa.

https://p.dw.com/p/1K6Vn
USA russicher Außenminister Sergei Lavrow beim UN-Generalversammlung
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, akilihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa mjini New YorkPicha: picture-alliance/dpa/J. Lane

Licha ya kuzozana vikali katika mkutano wa hapo jana, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wanatarajiwa kuongoza kwa pamoja mkutano wa mataifa 23 yanayounda kundi la msaada kwa Syria katika juhudi za mwisho za kufufua mkataba wa kusitisha mapigano nchini humo.

Mkutano huo wa leo unajiri baada ya pande hizo mbili kulaumiana kwa kuvuruga makubaliano ya kusitisha mapigano yaliokubaliwa mapema mwezi huu. Kila pande umeulaumu mwingine kwa ukiukaji wa mkataba huo.

Kerry ametoa wito kwa ndege zote za kivita kusitisha safari zake katika njia zinazotumiwa na mashirika ya misaada huku Lavrov akipendekeza siku tatu za kusitisha mapigano ili kufufua mkataba huo wa makubaliano ya kusitisha vita .

Hapo jana Kerry aliliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa anaitaka Urusi kuishinikiza Syria kulizuia jeshi lake kufanya mashambulizi yoyote, baada ya Marekani kulilaumu jeshi hilo kwa shambulizi dhidi ya magari ya misaada.

Lakini katika jibu lake, Lavrov alitangaza kuwa hakutakuwa na usitishaji wa upande mmoja tu wa jeshi la Syria na kuongeza kuwa wapiganaji wa upinzani hutumia fursa kama hiyo kupanga mashambulizi yao vizuri . Alisisitiza kuwa pande zote lazima zihusishwe kuhakikisha zinazingatia mkataba wa kusitisha mapigano na makundi ya kigaidi ambayo hayajaorodheshwa katika mkataba huo pia kuangaziwa upya.

Syrien Zivilbevölkerung in Aleppo
Raia nchini Syria wakitembea kando ya vifusi katika ngome ya waasi ya al-Sheikh Said karibu na Aleppo.Picha: Reuters/A. Ismail

Mapigano mapya yashuhudiwa Syria

Hayo yanajiri huku mapigano makali yakishuhudiwa hii leo viungani mwa mji wa Aleppo baada ya mashambulizi ya angani dhidi ya ngome za waasi usiku kucha na kusababisha mioto mikubwa.

Ni hali ya kusikitisha inayoendelea kushuhudiwa nchini humo na maswali mengi yakiwaghubika raia wasiokuwa na hatia, wengi wanajiuliza kimoyomoyo maswali yasiokuwa.

Wanaharakati wa upande wa upinzani waliilaumu serikali ya Syria na ile ya Urusi kwa kurusha mabomu hayo huku wazima moto wakujitolea wakipambana kudhibiti moto huo katika mji huo ambao tayari umeharibika.

Mashambulizi ya angani hapo jana yalisababisha vifo vya raia 12 wawili kati yao wakiwa watoto, hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya vifo mjini humo tangu kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mapema wiki hii.

Kusambaratika kwa mkataba huo wa kusitisha mapigano uliodhaminiwa na Marekani na Urusi kumesababisha mapigano mapya katika maeneo makubwa ya kivita nchini Syria katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa miaka mitano sasa.

Mwandishi :Tatu Karema/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga