Jeshi Myanmar latoa onyo kali dhidi ya waandamanaji
8 Februari 2021Majenerali wa kijeshi nchini Myanmar wametoa onyo kali leo dhidi ya muendelezo wa maandamano kupinga mapinduzi yaliyofanyika nchini humo mapema wiki iliyopita, mnamo wakati maelfu ya watu wakiandamana mitaani kushinikiza kuachiliwa huru kwa kiongozi aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi.
Sheria ya kijeshi imetangazwa leo katika baadhi ya maeneo ya mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar Mandalay. Hii ni baada ya mamia ya maelfu ya watu kuandamana sehemu mbalimbali nchini humo kupinga mapinduzi, huku jeshi likitoa onyo kali dhidi ya waandamanaji.
Sheria hiyo ya kijeshi inayopiga marufuku maandamano au mkusanyiko wa zaidi ya watu watano itatekelezwa katika mitaa saba ya mji wa Mandalay kati ya saa mbili usiku hadi kumi alfajiri. Jeshi limesema hayo kupitia taarifa.
Marufuku zaidi yatarajiwa dhidi ya waandamanaji
Sheria kama hiyo pia imetangazwa katika mji wa Ayeyarwaddy na matangazo mengine kama hayo pia yanatarajiwa kutolewa katika miji mingine usiku wa leo.
Huku wimbi la maandamano ya kupinga hatua ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika wiki iliyopita Myanmar likiendelea, kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali nchini humo MRTV, kimeripoti onyo kali kutoka kwa jeshi likisema upinzani dhidi ya jeshi ni kinyume cha sheria na unaashiria uwezekano wa kufanywa operesheni kali.
Taarifa hiyo ya kijeshi iliyosomwa kwenye kituo hicho ilieleza kwamba ni sharti hatua ichukuliwe kulingana na sheria kuhusu makosa yanayotatiza, yanayozuia au yanayoharibu utulivu wa nchi, usalama wa umma na utawala wa sheria.
Wito kwa UNHCR kuandaa kikao cha dharura kuhusu Myanmar
Hayo yakijiri,Umoja wa Ulaya na Uingereza zimelitaka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Haki za binadamu kuandaa kikao maalum kuhusiana na utata unaoikumba Myanmar.
Rais wa Marekani, Joe Biden amekuwa akiongoza miito ya kimataifa kulitaka jeshi kuachia madaraka na piakuachiwa huru kwa viongozi ambao wamewekwa kizuizini, akiwemo Aung San Suu Kyi.
Naye kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ametoa wito leo kutaka viongozi wa kisiasa wanaoshikiliwa waachiliwe huru mara moja.
Papa Francis ameuambia mkutano wa wanadiplomasia kwamba njia ya kuelekea demokrasia ambayo nchi hiyo ilichukua miaka ya hivi karibuni, inavurugwa zaidi na mapinduzi hayo.
Polisi watumia maji kuwatawanya waandamanaji
Tayari wanajeshi wameacha kutumia nguvu nyingi kujaribu kuzima maandamano yanayofanyika katika sehemu mbalimbali nchini humo. Lakini kufuatia kuongezeka kwa shinikizo maafisa wa polisi wamelazimika kutumia maji yanayowasha kuwatawanya maelfu ya waandamanaji waliokusanyika Naypyidaw.
Maandamano hayo yameendelea leo katika miji mbalimbali ikiwa ni mwanzo wa maandamano ya nchini kote.
Leo ni siku ya tatu ya maandamano ya nchi nzima kufuatia miito iliyotolewa na wanaharakati waliotaka pia wafanyakazi kugoma.
Katika mji wa Yangon ambao ni mji mkuu wa kibiashara, waandamanaji walijitokeza kwa wingi kuliko siku za nyuma huku wakijazana katika baadhi ya barabara kuu na kuzuia magari kupita.
San Suu Kyi na viongozi wengine wangali kizuizini
Wiki iliyopita, jeshi la Myanmar lilimuweka kizuizini Suu Kyi pamoja na viongozi wengine kadhaa wa chama chake cha Umoja wa Kitaifa kwa Demokrasia, hivyo kumaliza muongo mmoja wa utawala wa kiraia, lakini ni hatua iliyoshutumiwa pakubwa kimataifa.
Soma pia: Aung San Suu Kyi afunguliwa mashtaka baada ya mapinduzi
Wikendi iliyopita, maelfu ya watu waliandamana kupinga mapinduzi hayo. Hiyo ni licha ya hatua ya jeshi kuuzima mtandao wa intaneti.
Maandamano makubwa pia yameripotiwa katika miji iliyoko karibu na mpaka na China mfano Muse, Dawei na Hpa-an.
Majenerali wa Myanmar walimuweka kizuizini Suu Kyi aliye na umri wa miaka 75 Jumatatu wiki iliyopita, pamoja na viongozi wengine wa chama chake NLD, wakati wa mapinduzi wakidai uchaguzi uliopita ulikumbwa na udanganyifu.
(AFPE, RTRE)