Jeshi Myanmar lampinga ujumbe wa ASEAN
21 Februari 2022Jumuiya ya Mataifa 10 ya Kusini/mashariki mwa Asia, imekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha juhudi za kidiplomasia kumaliza mgogoro wa Myanmar ambao ulisababisha maandamano makubwa na ukandamizaji wa kikatili dhidi ya wapinzani wakiwemo takribani watu 12,000 ambao wametiwa mbaroni.
Hatua hiyo ina lengo la kuumaliza mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa takribani mwaka mmoja, tangu kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Cabodia, Prak Sokhon, mjumbe maalumu wa mataifa ya ASEAN kwa Myanmar, aliuambia ujumbe wa mawaziri wa kigeni kwamba alipanga kwenda Machi na kukutana na viongozi wa juu wa kijeshi. Lakini pia kukutana na kundi la wanachama wa serikali iliyoondolewa madarakani ya Aung San Suu Kyi ambayo inapigania kurejeshwa kwa serikali ya kiraia.
Sababu ya marufuku ya serikakali kwa mjumbe wa ASEAN
Lakini serikali ya kijeshi imezuia hatua hiyo kwa kusema haitaruhusu mjumbe huyo ajiusishe na makundi yanayoendeshwa kinyume cha sheria na kigaidi kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Myanmar. Na ikaongeza kusema pendekezo hilo "ni kinyume na kanuni za mkataba wa ASEAN lakini pia linadhoofisha juhudi za ASEAN za kukabiliana na ugaidi".
Mwezi Mei mwaka uliopita serikali ya kijeshi ya Myanmar ililitanga kundi la wabunge la serikali ya umoja wa kitaifa linalofahamika kwa kifupi kama NUG kuwa kundi la kigaidi, na kuwafunga maafisa wake kadhaa, ambao pia wako karibu zaidi na Suu Kyi. Idadi kubwa ya wanachama wa kundi hilo kwa sasa wanaishi uhamishoni au mafichoni na mjumbe Prak Sokhon hajatoa ufafanuzi wa wapi au lini mkutano ujao unaweza kufanyika.
Myanmar imekuwa katika machafuko, uchumi wake umevurugika na zaidi ya wakazi 1,500 wameuwawa baada ya kutokea kwa ukandamizaji wa kijeshi tangu mapinduzi ya Februari 2021.