Jeshi latoa saa 48 Misri
1 Julai 2013Katika taarifa yake iliyotangazwa kupitia televisheni, mkuu wa jeshi hilo Jenerali Abdel-Fatah el-Sisi amezitaka pande zote kusikiliza matakwa ya raia na kuongeza kuwa matakwa hayo yasipotekelezwa ndani ya masaa 48 yaliyotolewa, basi jeshi litalaazimika kutafuta suluhu yake lenyewe. Es-Sisi pia ameyaita maandamano ya siku ya Jumapili kuwa kielelezo kisio kifani cha matakwa ya umma.
Tamarod nayo yatoa muda wa mwisho
Vuguvugu linaloratibu kampeni ya kumuangusha rais Mursi la Tamarod lilisema katika taarifa iliyowekwa kwenye tovuti yake kuwa linampa rais huyo hadi Jumannne saa 11 jioni awe ameondoka madarakani na kuruhusu taasisi za kitaifa kuandaa uchaguzi wa mapema wa rais. Vinginevyo, liliongeza vuguvugu kuwa muda huo ndio utakuwa mwanzo wa kampeni ya uasi wa umma.
Afisa wa ngazi ya juu serikalini amesema kuwa mawaziri wanne -- wa Utalii, Mazingira, mawasiliano na masuala ya kisheria-- wamekabidhi barua zao za kujiuzulu kwa waziri mkuu Hisham Qandil. Hata hivyo, mawaziri wote waliojizulu si kutoka vyama vinavyomuunga mkono rais Mursi, lakini kujiuzulu kwao ni pigo kwa rais huyo, ambae tangu aingie madrakani amekuwa akipambana na idara ya mahakama, vyombo vya habari na polisi, ambavyo anavishtumu kwa kuhujumu juhudi za serikali yake.
Ofisi za udugu wa Kiislamu zachomwa moto na kuporwa
Baada ya maandamano ya Jumapili ambayo yalihudhuriwa na pande mbili za wafuasi na wapinzani wa Mursi, kulikuwepo na utulivu kiasi katika maeneo mengi ya nchi hiyo, lakini kuvamiwa kwa makao makuu ya chama cha Udugu wa Kiislamu na waandamanaji waliochoma ofisi hizo moto na kufanya uporaji, kumeonyesha kuongezeka kwa mgawanyiko nchini humo, na kukilaazimisha chama hicho kuzungumzia kuchukua hatua za kujilinda.
Watu wanane waliuawa katika mapigano ya usiku karibu na ofisi za chama cha Udugu wa Kiislamu, ambako walinzi waliwafyatulia risasi vijana waliokuwa wanarusha mabomu ya petroli na mawe, na afisa wa chama hicho alisema maafisa wake waili walijeruhiwa.
Mambo bado
Makundi hasimu yalishikilia misimamo yake baada ya kuonyeshana nguvu siku ya Jumapili katika uwanja wa Tahrir na katika maeneo mengine ya nchi. Waliberali walioandaa maandamano hayo walitangaza kuwa Mursi amepinduliwa na nguvu ya umma, lakini wakampa muda wa mwisho kuondoka ambao ni kesho Jumanne. Mursi ambaye hakuonekana mwenyewe, alirejea wito wa majadiliano na kuahidi kufanya kazi na bunge jipya litakalochaguliwa ikiwa mgogoro kuhusu sheria za uchaguzi utatatuliwa.
Lakini upinzani hauna imani na chama cha udugu wa Kiislamu, ambacho wanakituhumu kwa kutumia ushindi wake kadhaa katika chaguzi mbalimbali kujilimbikizia madaraka, na sasa wanataka kuwepo na muundo mpya kabisaa wa sheria za demokrasia ambazo wanasema zimepindishwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ofisi ya rais Mursi imesema itatoa taarifa majira ya saa tatu jioni.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Saum Yusuf