Jeshi la wanamaji la Senegal lawakamata wahamiaji 200
27 Julai 2024Msemaji wa jeshi amesema watu hao kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wamepelekwa mjini Dakar kwa ukaguzi zaidi.
Tukio hili linajiri siku chache baada ya watu 90 kufa maji kwenye pwani ya Mauritania walipokuwa wakijaribu kuvuka eneo hilo ili kuelekea barani Ulaya. Siku ya Jumatatu, takriban watu 25 walikufa katika ajali ya meli karibu na mji mkuu wa Mauritania Nouakchott.
Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko amewataka watu kutohatarisha maisha yao kwenye Bahari ya Atlantiki kwa kujaribu kuingia Ulaya. Lakini njia hiyo inazidi kutumiwa huku mamlaka zikiongeza ufuatiliaji katika Bahari ya Mediterania.
Soma pia: Wahamiaji 61 wapoteza maisha baharini njiani kwenda Ulaya
Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Uhispania la "Caminando Fronteras", katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo ya mwaka huu, zaidi ya watu 5,000 wamekufa wakijaribu kuwasili katika Visiwa vya Canary vya Uhispania.