1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lamshambulia kiongozi wa Hamas

31 Oktoba 2023

Jeshi la Israel limesema ndege zake za kivita zimemuuwa kamanda mwandamizi wa Hamas, ambaye anatajwa kuhusika na shambulizili la Oktoba 7 dhidi ya jamii mbili katika ardhi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4YECB
Israel Palästina I Gaza
Moshi unaonesha mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo la Rafah Ukanda wa GazaPicha: Ismael Mohamad/UPI/IMAGO

Katika taarifa ya pamoja ya Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) na Shirika la Usalama la Israeli (ISA) ambayo imesambazwa kupitia mtandao wa telegram, imemtaja Nasim Abu Ajina kuwa ni mtu aliyeongoza mauaji hayo ya Oktoba 7, katika maeneo ya Kibbutz Erez na Moshav Netiv HaAsara.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa kuuawa kwake kutaathiri kwa kiwango kikubwa jitihada ya kundi la Hamas, katika kuvuruga operesheni za kijeshi za jeshi la Israel. Mapema Asubuhi ya leo jeshi la Israel lilisema pia katika kipindi cha masaa 24 limeyashambulia maeneo 300, yakijumuisha mtambo wa kudhibiti mashambulizi ya vifaru na roketi, kadhalika wameshambulia pia mahandaki  ya wapiganaji wa kundi la Hamas.

Watu 800,000 wamekimbia Ukanda wa Gaza

Gazastreifen | Gaza Stadt nach israelischen Luftangriffen
Hali ya mashambulizi ya Israel katika maeneo ya mji wa GazaPicha: Abed Khaled/AP/dpa/picture alliance

Pasipo kutaja idadi, taarifa hiyo ya jeshi inasema wakati wa operesheni yake ya vikosi vya ardhini  idadi kadhaa ya wanamgambo wa Hamas waliuwawa. Aidha imesema takribani watu 800,000 wamekimbia eneo hilo lililozingirwa tangu kuzuka kwa mapigano majuma matatu yaliopita.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA)  Philippe Lazzarini anaelezea hali ilivyo kwa sasa huko Ukanda wa Gaza."Hakuna mahali salama katika Gaza. Hakuna raia waliosalia upande wa kaskzani ambao wanapata taarifa za uokozi kutoka kwa jeshi la Israel. Lakini wengi, wakiwemo wajawazito, watu wenye ulemavu, wagonjwa na waliojeruhiwa, hawawezi kuondoka. Kinachotokea na kinachoendelea kutokea ni kuwalazimika kuyahama makazi yao." Alisema afisa huyo.

Waziri Mkuu Netanyahu aapa kuliangamiza kundi la Hamas

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekaidi miito ya kimataifa ya kumtaka aache mapigano na kwa mara nyingine na ameonesha dhamira ya kulisambaratisha kundi la Hamas lenye kuitawala Gaza, au kufikisha kikomo kitisho cha kundi hilo kwa Israel baada ya uvamizi wa Oktoba 7.

Soma zaidi:Netanyahu apuuza miito ya usitishwaji mapigano

Zaidi ya nusu ya Wapalestina milioni 2.3 wa eneo hilo wameyakimbia makazi yao, ambapo maelfu wamepatiwa hifadhi katika shule zinaratibiwa na Umoja wa Mataifa au maeneo ya hospitali huku pia kukiwa na maelfu wengine waliojeruhiwa. Shirika, UNRWA limesema zaidi ya Wapalestina 672,000 wanahifadhiwa katika shule zao na maeneno mengine ikiwa ni mara nne zaidi ya uwezo wake.

Vyanzo: DPA/AP