Jeshi la Ethiopia larejesha udhibiti mji wa Lalibela
10 Novemba 2023Siku moja kabla, wapiganaji hao waliuteka Lalibela, mji ulio kwenye orodha ya turathi za dunia za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.
Mji wa Kihistoria wa Lalibela ulio katika mkoa wa Amhara na unaofahamika kwa makanisa yaliyojengwa miongo mingi iliyopita umeshuhudia mapigano ya mara kwa mara mwaka huu kati ya Wanajeshi wa Ethiopia na wanamgambo wa kundi la Fano.
Soma zaidi: Mgogoro wa Ethiopia watishia uthabiti wa kikanda-UN
Licha ya kuwa wanamgambo hao wanaopigana kwa kile wanachokiita "kujitetea" walishirikiana na vikosi vya nchi hiyo kwa miaka miwili katika vita kwenye jimbo la Tigray, mivutano imekuwa ikitokota baina yao baada ya Addis Ababa kutangaza mwezi Aprili kuwa, inasambaratisha makundi yote ya wapiganaji wa kieneo kote Ethiopia
Mapambano ya hivi karibuni yalianza Jumatano kwa kundi la Fano kuishikilia sehemu kubwa ya mji wa Lalibela, kulingana na maelezo ya wakaazi ambao hawakutaka kutajwa maina yao. Hata hivyo jana Alhamisi mkaazi mmoja alisema kuwa wapiganaji wa kundi hilo waliondoka usiku na kuwa hivi sasa jeshi ndilo linaloudhibiti mji huo.
Raia mwingine, alithibitisha kwa kusema kuwa hadi mapema asubuhi wanamgambo wa Fano walikuwepo katika sehemu kubwa ya mji lakini walipoamka wapiganaji hao walikuwa wakikamilisha harakati za kuondoka.
Wenyeji wa Lalibela wameeleza kuwa mapigano makali ya Jumatano yalisababisha vikosi vya jeshi la nchi hiyo kurudishwa nyuma katika kambi nje ya mji huo, ambao kulingana na takwimu rasmi una wakazi wasiopungua 37,000. Wawakilishi wa serikali ya Ethiopia hawakupatikana kuzungumza kuhusu hali mjini humo
Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed ilitangaza hali ya hatari mapema mwezi Agosti kwa kipindi cha miezi sita baada ya mapigano kuibuka katika mkoa wa Amhara.
Wasiwasi wa hali ya usalama waongezeka
Tangazo hilo limerejesha upya wasiwasi kuhusu hali ya utulivu miezi kadhaa baada ya makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya Tigray.
Mwezi Septemba, mamlaka ya haki za binadamu ya Ethiopia ilivituhumu vikosi vya jeshi la nchi hiyo kwa kuwakamata watu na kufanya mauaji holela, katika eneo la Amhara na maeneo mengine wakati kukiwa kumetangazwa hali ya hatari. Pamoja na kwamba mji wa Lalibela umejikuta kwenye mzozo wa hivi karibuni huko Amhara, eneo hilo lilikuwa pia kituo cha mapambano makali kati ya makundi hasimu wakati wa mzozo wa Tigray.