1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ethiopia lachukua tena udhibiti wa mji wa Lalibela

Saleh Mwanamilongo
20 Desemba 2021

Vikosi vya Ethiopia vimechukua tena udhibiti wa mji wa Lalibela, huku Kiongozi wa jimbo la Tigray akizilaumu Uturuki,Iran na Falme za Kiarabu kuchochea mgogoro nchini Ethiopia.

https://p.dw.com/p/44Yq5
Äthiopien | Norden | Rebellen Tigray
Picha: S.Getu/DW

Shirika hilo la habari la Ethiopia limeonyesha picha za naibu waziri mkuu akitembelea mji wa Lalibela. Hata hivyo, haijafahamika ni lini vikosi vya serikali vilichukua udhibiti wa mji huo, ulio na umuhimu mkubwa kwa Wakristo wa madhehebu ya Orthodoksi.

Wapiganaji wa kundi la ukombozi wa Tigray, TPLF waliuteka mji huo mnamo mwezi Agosti lakini vikosi vya serikali vilikabiliana na waasi hao mwanzoni mwa mwezi Disemba na kulazimisha  kuondoka.

Jumapili iliyopita, wakaazi waliripoti kwamba wapiganaji wa Tigray walichukua tena udhibiti wa mji huo baada ya jeshi na washirika wake kujiondoa.

''Majeshi ya kigeni yametenda uhalifu''

Rais wa Jimbo la Tigray Debretsion Gebremichael
Rais wa Jimbo la Tigray Debretsion GebremichaelPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Huku hayo ya kijiri, Rais wa jimbo la Tigray, Debretsion Gebremichael ameilaumu Uturuki, Iran na Falme za Kiarabu kwa kuuchochea mgogoro wa nchi hiyo kwa kutoa msaada wa kijeshi na kifedha kwa serikali.

Kituo cha televisheni cha Tigray kilimnukuu Gebremichael akisema mgogoro wa sasa wa Ethiopia umechochewa na kuingiliwa kati kutoka nje.

Amesema majeshi hayo ya kigeni na ya ndani yalikuwa yametenda uhalifu wa kivita, ambaye ameulinganisha na ''mauaji ya halaiki'' ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed dhidi ya watu wa Tigray.

Ndege za kijeshi na ndege zisizo na rubani za Ethiopia zimeshambulia maeneo mbalimbali jimboni

Tigray katika miezi ya hivi karibuni. Kwa upande wake serikali kuu ya Ethiopia imewalaumu wapiganaji wa Tigray kwa kuwaua raia na kuharibu miundombinu katika maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.

Ungwaji mkono wa Uturuki

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri MKuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri MKuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Emrah Yorulmaz/AA/picture alliance

Kauli hiyo ya kiongozi wa jimbo la Tigray imejiri wakati Waziri MKuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akihudhuria mkutano wa tatu wa Uturuki na Afrika huko Istanbul ambapo alisifu "mahusiano ya kihistoria" kati ya nchi mbili hizi.

Jana, Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia Abraham Belay alikutana na mwenzie wa Uturuki Hulusi Akar ambaye, kulingana na shirika la habari la Ethiopia, alimueleza kuhusu mafanikio katika teknolojia ya ulinzi ya Uturuki.

Ijumaa, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuunga mkono kuundwa jopo la watalaamu watakao chunguza vitendo vya kukiukwa haki za binadamu katika vita vya nchini Ethiopia vilivyoanza tangu Novemba mwaka jana.

Mzozo wa zaidi ya mwaka mmoja kati ya wapiganaji wa Tigray na vikosi vya serikali umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha maelfu ya wengine wakikabiliwa na baa la njaa.