Jeshi la Bangladesh laingia mtaani kuwadhibiti waandamanaji
20 Julai 2024Wanajeshi nchini Bangladesh wameendelea kushika doria katika miji mikubwa nchini humo ili kutuliza maandamano ya wanafunzi yanayozidi kuongezeka. Kwa upande mwingine polisi wa kutuliza ghasia wamewafyatulia risasi waandamanaji waliokaidi amri ya kutotoka nje iliyotolewa na serikali nchini humo mapema hii leo.
Soma zaidi. Polisi Bangladesh watoa amri mpya ya kutotoka nje
Ghasia za wiki hii zimesababisha vifo vya takriban watu 123 hadi sasa, kulingana na takwimu zilizoripotiwa na Shirika la habari la AFP. Amri ya kutotoka nje ilianza kutekelezwa usiku wa manane, ofisi ya Waziri Mkuu iliwataka wanajeshi kuingia barabarani kushika doria baada ya polisi kushindwa kuwadhibiti waandamanaji wanaopinga upendeleo katika kutolewa nafasi za ajira serikalini.
Tovuti za serikali na magazeti nchini humo yameshindwa kuchapisha taarifa kutokana na kizuizi cha mtandao kote nchini humo kilichowekwa tangu siku ya Alhamisi ambapo mpaka sasa bado kinatumika, Kizuizi hicho kimetatiza mawasiliano ndani na nje ya Bangladesh.