Ziara ya Blinken: Uhusiano wa Marekani na China kuboreka?
3 Februari 2023Takriban miezi mitatu baada ya mkutano wa kilele wa Bali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken atasafiri hadi Beijing Februari 5 kwa ziara ya siku mbili ili kuendeleza mazungumzo kati ya Washington na Beijing ambayo yanalenga kupunguza hali ya mvutano kati ya nchi hizo mbili na kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Marekani Joe Biden na kiongozi wa China Xi Jinping Novemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times, Blinken anatarajiwa kukutana na rais wa China Xi Jinping katika ziara yake ya siku mbili mjini Beijing. Wataalam hata hivyo wanasema safari hiyo itajikita kunako kile walichokiita "mambo jumla ya uhusiano" huku Blinken na waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gang wakijaribu kudumisha mawasiliano na kutafuta njia za kudhibiti kuzorota zaidi kwa uhusiano wa Marekani na China.
Soma zaidiBiden na Xi Jinping wakabiliana kwa simu:
Drew Thompson, Mtafiti mkuu katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore (NUS) na afisa wa zamani wa ulinzi wa Marekani amesema ajenda itakuwa ya kina na kwamba kila upande utakuwa na matakwa yake katika masuala yote yanayogubika uhusiano wa pande zote mbili.
Ingawa pande zote mbili zinatarajiwa kujadili orodha ndefu ya masuala, baadhi ya wachambuzi wanasema vita vinavyoendelea nchini Ukraine, mvutano unaoongezeka huko Taiwan na ushindani wa teknolojia ya juu kati ya Marekani na China huenda vikapewa kipaumbele. Sari Arho Havrén, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Helsinki na aliyebobea katika sera za kigeni za China amesema kwa upande wa Marekani, vita vya Urusi dhidi ya Ukraine hakika vitawekwa mezani.
Havrén ameiambia DW kuwa, Taiwan inasalia kuwa suala linalochukuliwa kama mstari mwekundu na Beijing na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang angependa kuona Blinken akithibitisha tena sera ya Marekani kuhusu China moja. Zaidi ya hayo, sera za Marekani za kuzuia makampuni ya Kichina kupata baadhi ya vifaa vya hali ya juu vinaweza pia kuwa kwenye ajenda.
Soma zaidi:Marekani yachunguza puto la Kijasusi la China kwenye angani
Matumaini hafifu ya kufikia maendeleo katika mahusiano hayo
Siku ya Jumanne, msemaji wa usalama wa taifa wa ikulu ya White House John Kirby alibaini kuwa Blinken atazungumzia vita vya Urusi nchini Ukraine wakati wa ziara yake mjini Beijing, na moja ya lengo kuu ya safari yake ni kufufua mawasiliano katika masuala ya kijeshi na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo yalisitishwa na Beijing baada ya ziara ya Spika wa zamani wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi huko Taiwan mwezi Agosti mwaka jana. Kirby amesema uhusiano baina ya Marekani na China ni muhimu zaidi duniani.
Soma zaidi: Maafisa waandamizi wa Marekani na China wakutana Zurich
Wakati huo huo, siku ya Jumatatu Wizara ya Mambo ya Nje ya China iliitaka Marekani kuzingatia mahusiano kati ya China na Marekani kwa kuwepo mazungumzo na ushirikiano vitakavyonufaisha pande zote, badala ya makabiliano na ushindani visivyo na tija.
Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Mao Ning, amesema wataendelea kutetea kwa uthabiti uhuru, usalama na maslahi yao na kwamba Beijing haitakwepa mashindano yoyote.
Wakati Blinken akijiandaa kwa ziara yake ya kwanza nchini China tangu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Washington pia inashirikiana na Japan pamoja na Uholanzi ili kujaribu kuweka vizuizi vipya vya kusafirisha zana za utengenezaji wa vifaa vya kiteknolojia kuelekea China, hatua ambayo Beijing ilisema ni mkakati wa Marekani wa kutumia vibaya udhibiti wa mauzo ya nje na kuweka siasa katika masuala ya teknolojia na biashara.