1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, ni wagombea wepi wanaowania uteuzi wa vyama Marekani?

25 Januari 2024

Wagombea wawili wanawania uteuzi wa chama cha Republican kuelekea uchaguzi mkuu wa Marekani utakaofanyika Novemba mwaka huu, huku Rais Joe Biden akitizamwa kuwa mgombea wa moja kwa moja wa chama cha Democratic.

https://p.dw.com/p/4bb4g
Ushindani wa uchaguzi mkuu uliopita kati ya Biden na Trump unatarajiwa kujirudia tena kwenye kampeni kuelekea uchaguzi wa Novemba 2024.
Ushindani wa uchaguzi mkuu uliopita kati ya Biden na Trump unatarajiwa kujirudia tena kwenye kampeni kuelekea uchaguzi wa Novemba 2024.

Rais Joe Biden wa chama cha Democratic ndiye rais aliye na umri mkubwa zaidi ambaye Marekani imewahi kuwa nayo. Huku kukiwa na wasiwasi kuhusu umri wake wa miaka 81, na ukadiriaji duni wa utendaji wake, atahitajika kuwashawishi wapiga kura kwamba angali ana nguvu ya kuwa rais kwa muhula mwingine wa miaka minne.

Kampeni ya Biden ya kugombea Urais

Washirika wa Biden wanasema anaamini kuwa yeye ndiye mgombea pekee wa Kidemokrasia anayeweza kumshinda Trump. Utafiti wa maoni wa hivi karibuni zaidi wa shirika la Reuters/Ipsos ulimpa asilimia 35, kiwango sawa na uungwaji mkono kwa Trump.

Alipotangaza nia yake ya kuwania kwa muhula wa pili, Biden aliweka bayana kwamba kazi yake ni kulinda demokrasia ya Marekani na akagusia shambulizi baya la Januari 6, mwaka 2021 dhidi ya bunge la Marekani Capitol Hill, lililofanywa na wafuasi wa rais wa zamani Donald Trump.

Biden ajinadi kama atakanyelinda demokrasia ya Marekani
Biden ajinadi kama atakanyelinda demokrasia ya MarekaniPicha: Eduardo Munoz/REUTERS

Suala la uchumi kwenye kampeni ya Biden

Kwa mara nyingine Kamala Harris ndiye atakuwa mgombea mwenza wake. Suala la uchumi litachangia pakubwa katika kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa tena.

Japo Marekani iliepuka mdororo wa uchumi uliotarajiwa na inakua kwa kasi zaidi kuliko wachumi walivyotarajia, mnamo mwaka 2022, mfumuko wa bei ulifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi shuhudiwa kwa miaka 40 iliyopita na gharama ya chakula na gesi inawalemea wapiga kura.

Biden ameongoza mwitikio wa serikali za nchi za Magharibi kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na kuwashawishi washirika kuiwekea vikwazo Moscow na kuunga mkono Kyiv, na amekuwa akiunga mkono Israeli katika mzozo wake na wapiganaji wa Hamas huko Gaza.

Hata hivyo, amekabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya chama chake kwa kushindwa kuunga mkono wito wa kusitisha mapigano eneo la Palestina, ambapo maafisa wa afya wa Gaza wanasema zaidi ya Watu 25,000 wameuawa.

Wachambuzi wampigia upati rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kushinda uteuzi wa chama cha Warepublican.
Wachambuzi wampigia upati rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kushinda uteuzi wa chama cha Warepublican.Picha: Kamil Krzaczynski/AFP/Getty Images

Donald Trump

Katika kinyang'anyiro cha tiketi ya chama cha Republican, rais wa zamani Donald Trump anakabiliwa na mashtaka manne ya uhalifu, hali ambayo haijawahi kutokea kwa rais wa zamani wa Marekani.

Hata hivyo, kesi hizo zimemuongezea umaarufu kati ya Warepublican.

Tayari amejizolea asilimia 49 ya uungwaji mkono katika chama chake, kulingana na utafiti wa maoni wa hivi punde uliofanywa na mshirika ya Reuters/Ipsos. Trump akaribia uteuzi wa chama chake huko New Hampshire

Alishinda mchujo wa kwanza katika jimbo la Iowa, ambapo alijikingia zaidi ya nusu ya kura zote.

Trump mwenye umri wa miaka 77, ametaja mashtaka dhidi yake kuwa ni njama za kisiasa kuhujumu azma yake kuwaniamuhula wa pili. Madai ambayo idara ya haki na sheria imapinga.

Ikiwa atachaguliwa tena, Trump ameapa kulipiza kisasi dhidi ya maadui zake. Amezidi kutumia lugha ya kimabavu, ikiwa ni pamoja na kusema atafanya kila jambo ili asiwe dikteta isipokuwa kwa "siku ya kwanza."

Biden: Kampeni ya "Fanya Marekani Kuwa Kuu Tena" ni tishio kwa demokrasia

Ameahidi kufanya mageuzi makubwa ikiwemo katika serikali ya shirikisho na kuwajumuisha watiifu wake, na kuweka sera kali za uhamiaji kama vile kuwafurusha wahamiaji kwa wingi na kufuta haki ya uraia kutokana na kuzaliwa Marekani. Ameahidi kufuta bima ya afya Obamacare iliyoanzishwa na mtangulizi wake Barrack Obama na pia kuweka vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya China.

Haley amepata umaarufu ndani ya chama chake kama mhafidhina thabiti mwenye uwezo wa kushughulikia masuala ya jinsia na jamii tofautitofauti kwa mtindo wa kuaminika zaidi.
Haley amepata umaarufu ndani ya chama chake kama mhafidhina thabiti mwenye uwezo wa kushughulikia masuala ya jinsia na jamii tofautitofauti kwa mtindo wa kuaminika zaidi.Picha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

Nikki Haley

Mwengine anayewania tiketi ya chama cha Republican ni Nikki Haley, gavana wa zamani wa jimbo la Carolina Kusini na ambaye alikuwa balozi wa Trump katika Umoja wa Mataifa.

Trump aongoza kinyang'anyiro cha kuwania urais

Haley mwenye umri wa miaka 52 amelipa kipaumbele suala la umri wake mdogo ikilinganishwa na Biden na Trump na vilevile historia yake kama binti wa mhamiaji wa Kihindi.

Haley amepata umaarufu ndani ya chama chake kama mhafidhina thabiti mwenye uwezo wa kushughulikia masuala ya jinsia na jamii tofautitofauti kwa mtindo wa kuaminika zaidi.

Pia anajinadi kama mtetezi shupavu wa maslahi ya Marekani kimataifa, na anapinga mtindo wa uongozi wa Trump akihoji ni wa machafuko sana na wa kugawanya jamii.

Wachambuzi wanahoji ushiriki wa Dean Phillips unaweza kumwathiri Joe Biden.
Wachambuzi wanahoji ushiriki wa Dean Phillips unaweza kumwathiri Joe Biden.Picha: Reba Saldanha/REUTERS

Wagombea wengine

Wagombea wengine wanaotafuta uteuzi ni pamoja na Marianne Williamson.

Dean Phillips mwenye umri wa miaka 55 anamezea mate tiketi ya chama cha Democratic, huku Robert F Kennedy Junior mwenye umri wa miaka 70 akiwa mgombea binafsi, sawa na Cornel West na Jill Stein

Chanzo: Reuters