1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Belarus inaelemea wapi zaidi kati ya Urusi na Magharibi?

Ibrahim Swaibu
19 Agosti 2020

Maandamano dhidi ya serikali yamekuwa yakishuhudiwa katika mji mkuu wa Belarus Minsk na katika miji mingine kwa zaidi ya wiki moja sasa. Lakini je, kwanini waandamanaji hawaonekani kupeperusha bendera ya Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3hChA
Minsk | Auftritt Lukaschenko Unabhängigkeitsplatz
Picha: Imago Images/ITAR-TASS/V. Sharifulin

Ukitazama ramani, utaona hali ya kipekee ya Belarus kijiografia. Upande wa Magharibi nchi hiyo inapakana na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami (NATO) ikiwemo Poland, Lithuania na Latvia na katika mpaka wake wa kusini, ni jrani na Ukraine, na kwa upande wa mashariki, Belarus ni jirani na Urusi.

"Lakini Belarus sio aina ya nchi ambayo inaweza kupunguza kitisho cha Urusi kwa Jumuiya ya NATO, anasema Gustav Gressel, mtaalamu katika Baraza la Ulaya linaloshughulikia  Masuala ya nje huku akiongeza kuwa nchi hiyo sio nchi ambayo haigemei upande wowote kama vile yalivyo mataifa ya Uswisi, Sweden au Finland.”

Gressel anasema Belarus ni nchi mwanachama ya Jumuiya ya  Mkataba wa Usalama wa Pamoja  (CSTO), Jumuiya ya  kijeshi ya mataifa sita ikiwemo pia Armenia,  Kazakhstan, Kyrgyzstan, pamoja na Tajikistan lakini kwa kiasi kikubwa inatawaliwa na Urusi.

Baada ya kufanya mazungmzo na rais wa Urusi Vladmir Putin, rais Lukashenko aligusia kuhusu Jumuiya hiyo pale alipoeleza kuwa huenda Urusi  itamuunga mkono mwanachama mwenzake wa (CSTO) katika kutuliza vuguvugu la maandamano.

Lukashenko ainyooshea kidole cha lawama NATO

Hatua ya Lukashenko kutaka Urusi kumuunga mkono ilijiri baada ya kiongozi huyo muimla kuelekeza kidole cha lawama kwa Jumuiya ya NATO kwa kile alichosema Jumuiya hiyo kupeleka wanajeshi katika mpaka wa Magharibi na taifa hilo, madai ambayo Jumuiya hiyo imekanusha.

"Tunaendelea kuwa makini na kuimarisha ulinzi wetu, tuko tayari kuzuiwa uvamizi wowote dhidi ya washiriki wetu,” amesema hapo Agosti 17, Jens Stoltenberg mkuu wa Jumuiya hiyo.

Katika hatua ya kuitikia uamuzi wa NATO rais Lukashenko aliamrisha kufanyika kwa zoezi la kijeshi karibu na mipaka ya Lithuania pamoja na Poland, hatua ambayo wachambuzi wanasema ni jaribio la kusababisha kitisho kutoka kwa mataifa ya kigeni ili kuishawishi Urusi kuingilia kati kijeshi.

Sio lazima kwamba Urusi inamuunga mkono Lukashenko

Gressel pamoja na wataalamu wengine wanaamini kuwa kwa sasa inaonekana kwamba Urusi haina matumaini makubwa katika Lukashenko, kiongozi wa kiimla ambaye katika wakati huu anaonekana kudhoofika.

Kulingana na wataalamu hao, ikulu ya Kremlin inaashiria kutojali kuhusu mabadiliko ya serikali maadamu serikali mpya haitabuni ushirikiano wa karibu na mataifa ya magharibi, Umoja wa Ulaya au Jumuiya ya Kujihamii NATO.

Wakati huo huo, inaonekana pia kuwa lengo kuu la vuguvugu la maandamano sio kujiunga na mashirirka hayo ya magharibi.

Upinzani nchini humo aidha haujatoa pendekezo la kutaka nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya, huku kiongozi wa upinzani Maria Kolesnikova akisema bado ni mapema mno Umoja huo kuwawekea vikwazo maafisa wa Belarus waliohusika katika vitendo vya kuwakandamiza waandamanaji. Anasema hatu hiyo itafifisha mchakato wa kufanya majadiliano kati ya upinzani na uongozi mjini Minsk.


Katika siku kadha wanadiplomasia katika Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya jijini Brusseles wa Ubelgiji wamekuwa wakionya kuhusu uwezekano wa kuipa Urusi mwanya wa kuulaumu Umoja huo  kwa kuingilia kati katika mambo ya ndani ya Belarus.

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema hapo Agosti 17 kuwa raia wa Belarus wana haki kuamua kuhusu maisha yao ya usoni na kumchagua kiongozi wanayemtaka kwa huru.

Wakizungumza kupitia njia ya simu hapo Agosti 18 rais wa Urusi Putin, na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walikubaliana kuhusu kutoingilia kati katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Chanzo: DW