Jacob Zuma ,Ethiopia na ICC Magazetini
4 Novemba 2016Tuanzie lakini Afrika kusini ambako gazeti la mjini Cologne,Kölner Stadt Anzeiger linaandika kuhusu kishindo cha rushwa kinachomkaba rais Jacob Zuma .Enzi za Jacob Zuma pengine hazitokawia kumalizika" linaandika gazeti hilo na kuzungumzia upinzani unaozidi kukuwa dhidi ya rais huyo anaeiongoza nchi ambayo uchumi wake unakumbwa na misuko suko. Kölner Stadt Anzeiger linasema ingawa Zuma bado hajenda kapa lakini wadadisi wengi wanaashiria mwisho wa enzi yake hauko mbali. Pigo la mwanzo limemsibu mapema wiki hii pale mwendesha mashitaka mkuu wa Afrika Kusini alipofutilia mbali mashitaka dhidi ya waziri wa fedha Pravin Gordhan. Hakuna asiyejua katika nchi hiyo ya Raas ya Matumaini mema kwamba Zuma alikuwa akitaka kwa kila hali kumtimua mwasiasa huyo anaeheshimiwa kwasababu ya kukosoa desturi mbaya zinazotumika serikalini pamoja na kupinga matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pigo la pili kubwa likafuata siku mbili baadae. Baada ya kuchapishwa ripoti inayobainisha wazi kabisa jinsi marafiki wa Zuma,wajasiria mali wenye asili ya India wanavyoshawishi maamuzi ya kuchaguiliwa mawaziri au hata viongozi wa mashirika ya umma mfano wa lile la nishati Eskom. Kamati huru itabidi iundwe katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja kuchunguza yaliyoandikwa ndani ya ripoti hiyo ya mpigania demokrasia bibi Thuli Madonsela. Muda mfupi kabla ya ripoti hiyo kuchapishwa maelefu waliandamana katika mji mkuu Pretoria kudai Zuma ajiuzulu. Linamaliza kuandika Kölner Stadt Anzeiger.
Ghadabu hazijatulia Ethiopia
Gazeti la die Tageszeitung limezungumzia hali nchini Ethiopia."Tusubiri hadi wimbi jengine la maandamano litakapopiga ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo la mjini Berlin. Linasema hata kama maandamano ya umati wa watu yamesita angalao kwa sasa,lakini katika ngome ya watu wa kabila la Amhara,pande zote mbili zinajiandaa kwa duru nyengine. Upande wa upinzani,linaendelea kuandika gazeti la die Tageszeitung,unahisi mageuzi yaliyoahidiwa na serikali ni hadaa tu.
ICC bado ni muhimu inasema Nigeria
Lilikuwa gazeti hilo hilo la die Tageszeitung lililozungumzia kuhusu msimamo bayana wa mataifa mengi ya Afrika kuelekea korti ya kimataifa ya uhalifu-ICC-mjini The Hague."Haki itasalia katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu inasema Nigeria na kupingana na hasimu yake Afrika Kusini" linaandika die Tageszeitung. Limemnukuu balozi wa Nigeria katika Umoja wa mataifa akiiyambia hadhara kuu mjini New York akisema Nigeria itaendelea kuwajibika na kushirikiana na korti hiyo ya kimataifa."Nigeria inaamini makosa yanabidi yaandamwe kokote kule ulimwenguni."
Vikosi vya kulinda amani havina uwezo
Na hatimae die Tageszeitung limeandika kuhusu kishindo wanachokabiliana nacho wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa."Peke yao wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa hawatoshi" linaandika gazeti hilo likimulika zaidi jukumu la vikosi hivyo nchini Sudan Kusini. Tume ya kulinda amani ya Umoja wa mataifa ifanye nini ikiwa malaki ya watu walioingiwa na woga,wanakwenda kuomba hifadhi lakini tume hiyo haina njia ya kuwasaidia? Katika nchi inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe,pande zinazopigana vita haziheshimu makubaliano ya amani wala maishja ya binaadam? Masuala yote hayo yametajwa hivi karibuni na kupelekea hatua kuchukuliwa.
Umuhimu wa kuundwa vikosi vya kuingilia kati haraka
Die Tageszeitung linakumbusha kwamba kutokana na ule ukwreli kwamba mfumo wa Umoja wa Mataifa hauruhusu makosa kutambuliwa na ni nadra pia uchunguzi kufanywa,hatua hii mpya inastahili sifa. Hata hivyo kuachishwa kazi kamanda wa vikosi vya kulinda amani sio jibu la suala la kimsingi vipi raia wanaweza kulindwa katika nchi inayogubikwa na vita."Tume za Umoja wa mataifa ni mchanganyiko wa vikosi kutoka kila pembe ya dunia na ni mchanganyiko wa watu wa tamaduni na uongozi tofauti wa kijeshi. Kwa hivyo katika suala la kukabiliana na mashambulio,,mtu anaweza kusema hawafai. Na kutokana na kuzidi mashambulio dhidi ya raia,kuna haja kubwa ya kuwa na vikosi vya kuingilia kati.Tume ya Umoja wa mataifa ambayo haiwezi kufanya hivyo,inageuka kuwa mtihani badala ya ufumbuzi.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse
Mhariri:Yusuf Saumu