1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

081211 UN-Klimagipfel Durban

Oliver Samson8 Desemba 2011

Kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo yanayofanywa na Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa tabia nchi. Shinikzo limeongezeka, kwa sababu wataalamu wanaonya kuhusu athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

https://p.dw.com/p/13Os9
Jacob Zuma
Rai wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Mbuyu ni mti uliochaguliwa kuwa alama ya mkutano wa Umoja wa Mataifa unaouhusu masuala ya tabia ya nchi unaofanyika Durban, Afrika ya Kusini. Kiutamaduni viongozi wa Kiafrika walikutana chini ya mbuyu na kufanya majadiliano mpaka kufikia muafaka.

Mkutano wa Durban unafanyika katika kipindi cha siku nne. Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anafahamu fika kwamba muda huo hautoshi kufikia muafaka na hivyo amewawekea shinikizo mawaziri waliohudhuria mkutano huo, ili angalau kunusuru makubaliano yaliyoafikiwa katika itifaki ya Kyotto. Mpango wa Zuma unaungwa mkono na Umoja wa Ulaya pamoja na serikali ya Ujerumani, kama alivyoeleza waziri wa mazingira wa nchi hiyo, Norbert Röttgen, katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano huo wa Durban.

Norbert Röttgen
Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Norbert RöttgenPicha: picture-alliance/dpa

"Umoja wa Ulaya na Ujerumani zinayafuata mapatano Kyotto. Tunataka mapatano hayo pamoja na mfumo mzima ulioafikiwa uendelee kukua," alisema Röttgen. "Itifaki ya Kyotto pamoja na ahadi zinazotolewa na nchi mbali mbali ndio njia ya nzuri ya kupunguza hewa chafu. Huu ni msingi wa sheria ya ndani za Umoja wa Ulaya ambayo itafanya kazi hadi 2020."

Shinikizo la Umoja wa Ulaya na la Afrika ya Kusini litaweza kusaidia kuendeleza mazungumzo na pia kuwezesha kuanzishwa kwa kipindi cha pili cha kutekeleza makubaliano ya Kyotto. Mtaalamu wa shirika la Greenpeace linalohusika na uhifadhi wa mazingira, Bw. Martin Kaiser, anaeleza kwamba hayo ndio madai ya rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.

Kwa upande mmoja Zuma amesama kwamba itifaki ya Kyoto lazima ifuatiwe na kipindi cha pili cha utekelezaji kitakachofuatiliwa kisheria," alisema mtaalamu huyo. "Hapa ndipo ambapo Umoja wa Ulaya unatakiwa kushughulika. Lakini anasema pia kwamba wakati huohuo panatakiwa pawepo na majadiliano yanayohusisha nchi zinazochafua hewa kwa kiasi kikubwa kama vile China na Marekani. Tunahitaji maamuzi na tarehe ambayo maamuzi hayo yataanza kufuatwa."

Mtaalamu huyo anaendelea kusema kwamba ni lazima kuhakikishwa kwamba kipindi cha kufuata mapatano ya kyotto kinachokwisha 2012, kitafuatwa na kipindi cha pili.

Naye waziri wa mazingira wa Ujerumani, Norbert Röttgen alisema kwamba Umoja wa Ulaya umeshachuka hatua lakini umoja huo pamoja na nchi chache nyingine zilizotayari kuendelea kutekeleza mapatano ya Kyotto hazitaweza kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi. Röttgen amesema kwamba ni lazima nchi zinazotoa hewa chafu kwa wingi nazo ziwe tayari kujiwajibisha. Aliongeza kuwa Ujerumani imeweka mpango wa kubadilisha matumzi ya nishati ili kupunguza utoaji wa hewa chafu kwa asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 1990.

Siku mbili zijazo zitadhihirisha kama msukumo wa Umoja wa Ulaya utasaidia kuwekwa kwa malengo ya kupunguza hewa chafu na kama patakuwa na kipindi cha pili cha kutekeleza mapatano ya Kyotto.

Mwandishi: Jeppesen, Helle/Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Khelef