1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jacob Zuma atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa

Gregoire Nijimbere20 Juni 2005

Aliyekuwa makamu wa rais wa Afrika ya kusini, Jacob Zuma, atafikishwa mbele ya mahakama kwa shutuma za ulaji rushwa. Hiyo ndiyo hatua ya kisheria ambayo imefuatia hatua ya hivi majuzi ya rais Thabo Mbeki ya kumfuta kazi aliyekuwa msaidizi wake.

https://p.dw.com/p/CHgN

Muda mfupi uliopita, msemaji wa mwendesha mashitaka mkuu wa jamhuri nchini Afrika ya kusini Makhosini Nkosi, amewaambia waandishi habari kwamba, wamechukuwa hatua ya kumfikisha mbele ya mahakama ya jinai Jacob Zuma.

Bwana Nkosi amesema “katika hali kama hii ambapo kuna ushahidi thabiti, tunafikiri tuna sababu ya kuifikisha kesi mahakamani. Zuma ajiandae kuyajibu mashitaka mahakamani wakati wowote ule mnamo wiki hii”.

Kulingana na msemaji huyo, hatua hiyo imechukuliwa baada ya mwendesha mashitaka mkuu Vusi Pikoli kumuarifu Zuma kuhusu hatua hiyo ili akusanye ushahidi wa kujitetea.

Rais Thabo Mbeki, alimfukuza makamu wake wiki jana baada ya msaidizi wa Zuma katika maswala ya kifedha Schabir Shaik kupatikana na hatia na korti kuu ya mjini Durban mwezi huu, katika njama mbili za ulaji rushwa, kwa manufaa ya Zuma.

Schabir Shaik, tayari alikatiwa adhabu ya kifungo cha miaka 15.

Hatia ya kwanza ni kumpangia njama ya rushwa Zuma wa laki 5 za Randi, sawa na elfu 72 na mia 5 ya dola za kimarekani kutoka kwa kampuni mojawapo ya silaha ya Ufaransa kama malipo ya kuifadhi kampuni hiyo mnamo miaka ya 90 ambapo kulifanyika biashara kubwa ya silaha nchini Afrika ya kusini katika hali ya sintofahamu.

Hatia ya pili ni Shaik mwenyewe, kumkabidhi Zuma milioni 1 na laki 3 za Randi, ikiwa ni sawa na laki 2 za dola za kimarekani ili kunufaika na ushawishi wa Zuma kama makamu wa rais katika biashara yake binafsi.

Bwana Jacob Zuma alinusurika katika tuhuma za ulaji rushwa miaka miwili iliopita.

Nchini Afrika ya kusini, mkasa huo wa Zuma umetafsiriwa kwa njia tofauti. Baadhi ya wanasiasa hata ndani ya chama tawala cha African National Congres ANC, ambako Zuma bado ana washabiki wengi kama makamu mwenyekiti wa chama, wanadai kuwa hii ni njama ya kisiasa ya kumzuwia Zuma kuuwania kiti cha urais.

Hadi wakati huu, Zuma alikuwa akizingatiwa kama yule atakayemrithi Thabo Mbeki katika uchaguzi utakaofanyika ifikapo mwaka wa 2009.

Wengine wanaona kuwa kumfukuza makamu wake, rais Mbeki ameonyesha nia na utashi wake wa kupambana na rushwa. Hiyo itakuwa hoja kubwa kwa nchi 8 tajiri ambazo zinatarajiwa kukutana mwezi kesho kujadili mipango ya kuisaidia Afrika na ambazo mara kwa mara zinatoa sharti la kuondoa rushwa.

Tom Lodge mhadhiri wa maswala ya kisiasa kwenye chuo kikuu cha Witwatersrand mjini Johannesburg, amesema kwamba “Watu wema wanaotaka kusaidia wakikasirishwa lakini na rushwa na uongozi mbaya, watafurahia hatua hiyo”.