240210 Deutsche Literatur
25 Februari 2010
Kuna taasisi kadhaa nchini Ujerumani zinazoshughulikia uenezaji wa fasihi ya kijerumani duniani.Na muhimu kati ya taasisi hizo ni chuo cha Goethe.
Katika muda wa miaka mingi taasisi hiyo imesimamia tafsiri za vitabu karibu alfu tano kutoka nyanja mbalimbali za fasihi.
Ujerumani imebarikiwa kuwa na waandishi mashuhuri wa riwaya, vitabu vya sayansi na vitabu vya fasihi ya watoto.
Bertold Brecht ni miongoni mwa waandishi hao mashuhuri katika tanzu ya tamthilia.
Sabine Erlenwein anaeshughulikia kazi za tafsiri ya vitabu kwenye chuo cha Goethe anasema wapo waandishi ambao hawawezi kupitwa kama vile Günther Grass lakini amesema pana orodha ndefu ya waandishi wa zama za leo.
Miongoni mwa vitabu vilivyotafsiriwa ni vile vya Daniel Kelhmann , mwandishi wa riwaya maaruf inayoitwa "kipimo cha dunia"- Kazi za mwandishi huyo zimetafsiriwa katika lugha 41 .
Erlenwein anaeshughulikia tafsiri hizo amefuatilia kwa muda wa miaka ya hivi karibuni jinsi fasihi ya kijerumani inavyorejea tena katika medani ya kimataifa hasa kutokana na kuanzishwa kwa tuzo ya uandishi wa vitabu ambayo inatolewa tokea mwaka wa 2005.
Rika jipya la waandishi limejijenga nchini Ujerumani.
Miongoni mwa wa waandishi hao ni Sasa Stanisic alieandika kitabu maaruf juu ya wakimbizi wa vita vya Bosnia.
Vitabu vyake vinauzwa kwa leseni katika nchi 20 .
Juu ya kurejea kwa fasihi ya kijerumani katika medani ya kimataifa msimamizi wa kazi za tafsiri kwenye chuo cha Goethe bibi Sabine Erlenwein amesema fasihi hiyo imefana katika Ulaya ya kati na ya mashariki.
Hatahivyo ameelaza kwamba fasihi hiyo inakabiliwa na ushindani mkubwa katika nchi ambapo lugha ya kiingereza inatumika.
Taasisi ya Goethe inatafsiri vitabu kati ya 250 na 300 kila mwaka, na kwa ajili hiyo kitengo cha ufasiri vitabu kinapata kiasi cha Euro laki tano hadi sita kila mwaka.
Lakini chuo cha Goethe kina mustakabali mzuri kutokana na waandishi wake wa kisasa.
Wasomaji vitabu duniani kote wana uchu wa kusoma vitabu vya waandishi wa kijerumani.
Mwandishi/Cordsen Knut/ZA
Imetafsiriwa na Mtullya Abdu/
Mhariri/Abdul-Rahman,Mohammed