1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoIvory Coast

Ivory Coast ukingoni mwa kutolewa nje ya michuano ya AFCON

23 Januari 2024

Wenyeji Ivory Coast watalazimika kusubiri nusra kwa kutegemea matokeo mengine ili kuepuka kuondolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON.

https://p.dw.com/p/4bZRz
Wachezaji wa Ivory Coast | AFCON
Wachezaji wa Ivory CoastPicha: Franck Fife/AFP/Getty Images

Hii ni baada ya kupokea kichapo cha mbwa kuingia msikitini kwa kufungwa mabao 4-0 na Guinea ya Ikweta katika mechi ya mwisho ya kundi A.

Mabao mawili ya Emilio Nsue, na mpira wa kutengwa uliotiwa kambani na Pablo Ganet na bao la dakika za mwisho la Yannick Buyla yalitosha kuwazamisha wenyeji na kuhakikisha kuwa vijana wanaotiwa makali na kocha Juan Micha wanamaliza kileleni mwa kundi A wakiwa na alama 7.

Kwa wakati huu, wenyeji Ivory Coast wanasubiri nusra tu ambayo nayo haina uhakika wa kuja, ili kufuzu katika hatua ya 16 bora baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu wakijikingia alama tatu pekee.

Soma pia: Je, michuano ya AFCON mwaka 2024 itakuwa ya ushindani zaidi?

Zipo nafasi nne zinazotolewa kwa timu zilizoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora kwenye makundi kufuzu katika raundi ya mtoano.

Baadhi ya wachezaji wa Ivory Coast walikuwa wakibubujikwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho huku wakizomewa na mashabiki wao wa nyumbani katika dimba la Alassane Ouattara.

Guinea ya Ikweta yaandika historia

Wachezaji wa Guinea ya Ikweta wakisherehekea ushindi wao dhidi ya Ivory Coast
Wachezaji wa Guinea ya Ikweta wakisherehekea ushindi wao dhidi ya Ivory CoastPicha: Ebenezer Amoakoh Photogod/Samuello Sports Images

Guinea ya Ikweta kwa upande wao, walisherehekea ushindi huo kwa mbwembwe baada ya kuandikisha ushindi wa kihistoria katika michuano ya AFCON na sasa itamenyamana na timu iliyomaliza katika nafasi ya tatu aidha kutoka kundi C, D, au E katika hatua ya mtoano siku ya Jumapili.

Mara ya mwisho kwa vijana wa Guinea ya Ikweta kufika mbali katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ilikuwa mwaka 2015 walipotia guu hadi nusu fainali.

Ama kwa upande mwengine, Misri imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kutoka sare ya 2-2 na Cape Verde katika mechi ya kundi B.

Soma pia: Kombe la Afrika: Nyota wa soka wawa mashujaa wa kitaifa

Misri, iliyokuwa bila ya nyota wao Mohamed Salah, imefuzu licha ya kutoka sare katika mechi zake tatu ilizocheza.

Kwengineko, Nigeria ilipata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Guinea Bissau na kujikatia tiketi ya raundi ya 16 bora. Super Eagles imeungana na Guinea ya Ikweta kufuzu katika raundi ya 16 bora baada ya kujizolea alama 7 katika michezo mitatu.

Katika kundi B, mabingwa mara nne wa AFCON Ghana ilitoka sare ya 2-2 na Msumbiji na sasa hatma yao kufuzu haiko tena mikononi mwao.

The Black Stars kama wanavyojulikana kwa jina la utani, inasubiri miujiza kusonga mbele kama moja ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu.

Michuano hiyo inaendelea tena leo huku Guinea ikicheza na bingwa mtetezi Senegal, Gambia ikiwa na kibarua dhidi ya Cameroon, Mauritania watakabana koo na Algeria kabla ya Angola kumaliza udhia na Burkina Faso.