Israel yazidi kushinikizwa isiivamie Rafah
16 Februari 2024Ikulu ya White House, ilisema Rais Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jioni ya Alhamis (Februari 15) na kumtaka kutofanya mashambulizi mjini Rafah bila ya mpango wa kuhakikisha usalama wa raia katika eneo hilo.
Ujerumani, Uingereza, Australia, Canada na New Zealand pia zimeitaka Israel kutofanya mashambulizi ya ardhini katika mji huo wa Rafah.
Soma zaidi: Viongozi wa dunia waisihi Israel kuacha operesheni ya Rafah
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak imesema kwamba kiongozi huyo amemwambia Netanyahu kwa njia ya simu kwamba Uingereza ina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuzuka janga la kibinaadamu kutokana na uvamizi wa kijeshi mjini Rafah.
Hata hivyo, Netanyahu amesisitiza kuwa ataendelea na operesheni katika mji huo wenye idadi kubwa ya watu hadi atakapopata ushindi kamili dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas.