1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yawaachilia wafungwa 90 wa Kipalestina

20 Januari 2025

Israel imewaachilia wafungwa 90 wa Kipalestina leo Jumatatu baada ya Hamas kuwaachilia mateka watatu wa Israel siku ya Jumapili na kukamilisha mabadilisho ya kwanza chini ya mpango wa kusitisha vita.

https://p.dw.com/p/4pMcZ
Israel Reim 2025 | Hamas yawaachilia mateka wa Israel
Doron Steinbrecher, (kushoto) akiwa amekumbatiana na mama yake Simona baada ya Doron kuachiliwa na kundi la Hamas Januari 19, 2025Picha: Israeli Army/AP/picture alliance

Vita katika Ukanda wa Gaza vimedumu kwa zaidi ya miezi 15.

Mateka watatu wa Israel walioachiliwa wote ni wanawake na tayari wameungana na familia zao baada ya kupelekwa hospitali kuchunguzwa afya zao. Madaktari wamesema wote watatu wapo katika hali nzuri ya kiafya.

Na saa chache baadaye Israel nayo iliwaachilia wafungwa wa Kipalestina waliokuwa katika gereza la Ofer lililopo katika eneo la Ukingo wa Magharibi na kuwasafirisha kwa mabasi.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kuanza kwa mabadilishano hayo kunatoa matumaini kwamba mateka wengine pia wataachiliwa.

Katika mpango wa makubaliano ya awali ni kwamba jumla ya mateka 33 wa Israel, wanatarajiwa kurejeshwa kutoka Gaza. 31 kati yao ni wale waliochukuliwa na wanamgambo wa Hamas wakati wa mashambulio ya Oktoba 7, 2023. Israel itawaachia wafungwa wa Kipalestina wapatao 1,900.