1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yauwa Wapalestina zaidi ya 100, yajeruhi zaidi ya 700

1 Machi 2024

Wizara ya afya kwenye Ukanda wa Gaza ilisema jeshi la Israel liliwamiminia risasi na kuwauwa Wapalestina 104 na kuwajeruhi wengine 760 wakati wakifuatilia gari la misaada ya chakula, tuhuma zilizokanushwa na jeshi hilo.

https://p.dw.com/p/4d43d
Ukanda wa Gaza mauaji kwenye msaada wa chakula
Picha ikionesha jinsi wanajeshi wa Israel walivyowalenga Wapalestina waliokuwa wamezunguka malori yenye misaada ya chakula katika kile ambacho jeshi hilo lilisema wanajeshi wake walidhani ni kitisho kwao siku ya tarehe 29 Februari 2024.Picha: Anadolu/picture alliance

Kulingana na wizara hiyo, mauaji hayo yalifanyika wakati Wapalestina walipokuwa wakipewa misaada ya chakula.

Lakini msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, alikanusha tuhuma hizo akisema wanajeshi wao hawakumshambulia mtu yeyote kimakusudi, bali yalikuwa maafa yaliyosababishwa na mkanyagano.

Soma zaidi: Hizbullah yakabiliana kijeshi na Israel

Hagari alidai kuwa wakati misaada hiyo muhimu ya kibinaadamu ilipokuwa ikielekea kwa watu wenye mahitaji, maelfu ya watu waliyakimbilia malori.

"Wengine walianza kusukuma kwa nguvu na kuwakanyaga wengine hadi kufa, huku wakipora misaada ya kibinadaamu," alidai msemaji huyo wa jeshi la Israel akilitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha na lililosababisha "makumi ya Wagaza kuuawa na kujeruhiwa."

Wizara ya Afya ya Gaza inasema idadi ya watu waliouawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza imepindukia 30,000.