1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatuhumiwa kuihujumu Syria

8 Desemba 2014

Syria inaituhumu Israel kufanya mashambulio mawili ya angani dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali karibu na mji mkuu Damascus,ikidai Israel "inawaunga mkono moja kwa moja" waasi na wanamgambo wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/1E0j8
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: Reuters/Sana

"Jumapili jioni,jeshi la Israel limehujumu maeneo mawili yaliyokombolewa na serikali katika mkoa wa Damascus:eneo la kaskazini magharibi la Dimas na lile la uwanja wa ndege wa Damascus"jeshi la Syria limesema katika taarifa yake iliyotangazwa katika televisheni na kuongeza hakuna hasara iliyopatikana.

Wizara ya mambo ya nchi za nje wa Syria imesema jana usiku wamemtaka katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon na baraza la usalama la Umoja wa mataifa waiwekee vikwazo Israel.Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Syria imezitaja hujuma hizo za Israel kuwa ni "uhalifu mkubwa dhidi ya mamlaka ya Syria."

Kwa mujibu wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadamu la Syria-eneo la Dimas ni la kijeshi na uwanja wa ndege wa Damascus unasimamiwa sehemu moja na jeshi na ya pili na raia."Hujuma za Israel zimelengwa kuwasaidia magaidi nchini Syria baada ya vikosi vyetu kuondoka na ushindi huko Deir Ezzor,Alleppo na kwengineko"-taarifa ya jeshi imesema."Ni ushahidi Israel inawaunga mkono moja kwa moja magaidi nchini Syria."

Serikali ya Syria inatumia neno magaidi kumaanisha waasi na pia wafuasi wa itikadi kali.

Israel haijakanusha wala kuthibitisha

Viongozi wa Israel hawakusema chochote kuhusu mashambulio hayo hadi sasa.Hata hivyo waziri wa upelelezi Youval Steinitz amesema nchi yake imepania kuzuwia harakati zozote za kusafirisha silaha za kimambo leo za Syria hadi Libnan.Amekataa lakini kuthibitisha au kukanusha mashambulio ya angani dhidi ya Syria.

International Airport in Damaskus
Kiwanja cha ndege cha kimataifa mjini DamascusPicha: Getty Images/AFP/Louai Beshara

Jeshi na madege ya kivita ya Israel yamefanya mashambulio kadhaa dhidi ya vituo vya Syria tangu uasi dhidi ya utawala wa rais Assad ulipoanza marchi mwaka 2011.Madege ya kivita ya Israel yamehujumu pia miundo mbinu ya chama cha Hisbollah cha Libnan au silaha walizokusudiwa.

Taarifa kuhusu mashambulio ya jana,zimetolewa katika wakati ambapo vikosi vya serikali vimefanikiwa kuyakomboa maeneo kadhaa mnamo muda wa masaa 24 yaliyopita.Kwa mujibu wa shirika linalosimamia haki za binaadam la Syria,vikosi vya serikali vimefanikiwa pia kuzuwia shambulio la wanamgambo wa dola ya kiislam dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi huko Deir Ezzor,ambapo zaidi ya wanajihadi 100 na wanamgambo 59 wameuliwa.

Jeshi la serikali linawazingira waasi

Wakati huo huo jeshi linasonga mbele katika mkoa wa Aleppo ambako kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binaadam waasi 24 na wanajihadi wameuliwa kaskazini ya mji huo.Jeshi la serikali limeuteka mji wa Breij-mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema aliyeongeza jeshi linawazingira waasi mashariki ya Aleppo-mji wa pili mkubwa nchini Syria.

Syrien Kämpfe in Deiz ez-Zor Militärflughafen Juni 2013
Mapigano katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Deiz ez ZorPicha: Ahmad Aboud/AFP/Getty Images

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri