Israel yasema muungano wa kanda watibua shambulizi la Iran
20 Juni 2022Waziri Gantz amesema anatarajia ziara ijayo ya rais wa Marekani Joe Biden katika eneo itaimarisha zaidi muungano huo. Katika taarifa kwa kamati ya bunge ya mambo ya nje na ulinzi yenye ushawishi, Gantz ametoa maelezo machache kuhusu Muungano huo wa Ulinzi wa Anga wa Mashariki ya Kati ikijumuisha kile ambacho nchi nyingine ni sehemu yake.
Gantz amesema muungano huo ni hatua ya kwanza ya maono ya pamoja wakati kukiwa na jaribio la mashambulizi ya Iran dhidi ya mataifa ya kanda hiyo kwa kutumia roketi, makombora na ndege zisizo na rubani.
Muungano wawezesha kutibuliwa kwa shambulizi la Iran
Gantz ameongeza kuwa mpango huo tayari umewezesha kutibuliwa kwa ufanisi kwa jaribio la Iran la kuivamia Israeli na mataifa mengine. Ameongeza kuwa ziara ya Biden inayojumuisha ziara nchini Israel na Saudia Arabia katikati ya mwezi Julai, pia itasaidia katika mchakato huo.
Israel inaichukulia Iran kuwa adui wake mkubwa. Miaka miwili iliyopita, ilianzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain, nchi mbili za Kiarabu za Ghuba ambazo pia zinahisi kutishiwa na
Iran. Pia inaaminika kuwa na uhusiano usiokuwa wazi na Saudi Arabia uhusiano ambao Israel inatumai kuwa ziara ya Biden inaweza kuimarisha.