1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema imeyakamata majengo ya Bunge la Gaza

14 Novemba 2023

Jeshi la Israel limesema limeyakamata majengo ya Bunge la Gaza na taasisi nyingine za serikali ya Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza wakati vikosi vyake vinatanua operesheni ya kijeshi ndani ya ardhi hiyo.

https://p.dw.com/p/4Yo1S
Zerstörtes palästinensisches Parlament in Gaza Stadt
Picha: Maxppp Wissam Nassar/dpa/picture-alliance

Jeshi la Israel limesema leo kuwa limeyakamata majengo ya Bunge la Gaza na taasisi nyingine za serikali inayoongozwa na kundi la Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza katika wakati vikosi vyake vinatanua operesheni ya kijeshi ndani ya ardhi hiyo ya Palestina.

Taarifa ya jeshi hilo imesema wapiganaji wake wamechukua udhibiti wa Bunge la Hamas, jengo kuu la serikali, makao makuu ya polisi na taasisi moja ya masuala ya uhandisi ambayo Israel inasema "ilikuwa inatumika kutoa ujuzi wa kuunda makombora."

Hayo yameripotiwa wakati Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imesema imelazimika kuizika kwenye kaburi la pamoja miili ya watu 180 iliyoanza kuharibika ikiwa imehifadhiwa chini ya majengo ya hospitali kubwa ya Al-Shifa.

Viunga karibu na hospitali hiyo inayodhaniwa kuwahifadhi maelfu ya wapalestina wanaokimbia vita,  vimegeuka uwanja wa mapambano kati ya jeshi la Israel na wapiganaji wa kundi la Hamas.