Israel yakanusha vikosi vyake kuingia Syria
10 Desemba 2024Hii ni baada ya vyanzo vya Syria kusema uvamizi wa Israel umeingia hadi umbali wa kilomita 25 kutoka mji mkuu Damascus. Baada ya utawala wa miongo mitano wa Assad kuangushwa Jumapili, askari wa Israel waliingia katika eneo lisilo na wanajeshi ndani ya Syria, lililowekwa kufuatia vita vya mwaka wa 1973.
Israel inasema uvamizi huo ni hatua ya muda kuhakikisha usalama wa mpakani. Luteni Kanali Nadav Shoshani, msemaji wa jeshi la Israel amesema askari walibaki katika eneo la ulinzi na maeneo mengine machache yaliyo karibu, lakini akakanusha kuwa walijaribu kuingia ndani kabisa ya Syria mbali na eneo hilo la milima ya Golan.
Wakati huo huo, waasi wa Syria ambao sasa wako madarakani mjini Damascus wamemteuwa Mohammad al-Bashir kuwa mkuu wa serikali ya mpito. Vyombo vya habari vya serikali vimesema serikali hiyo itahudumu hadi Machi mosi.