Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza
17 Julai 2024Msemaji wa shirika la ulinzi wa kiraia wa Gaza Mahmud Bassal amesema mashambulizi hayo matatu ya angani yamesababisha vifo vya takriban watu 44 na kujeruhi wengine ndani ya saa moja katika eneo lililokumbwa na vita la Palestina. Hata hivyo Israel ilithibitisha kufanya mashambulizi mawili.
Wizara ya afya ya Gaza imeripoti shambulizi katika kituo cha mafuta, huko Al-Mawasi kusini mwa Gaza na kuwauwa watu 17, huku shirika la Hilali Nyekundu la Palestina ikiripoti shambulizi jengine katika Shule ya Al-Razi inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza na kusabisha vifo vya watu watano.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiapa kuongeza shinikizo kwa Hamas.
Wizara ya Afya Gaza yasema watu 38,664 wameuawa tangu kuanza vita
"Huu ndio wakati mahsusi wa kuongeza shinikizo zaidi, kuwarudisha nyumbani mateka wote, walio hai na waliokufa na kufikia malengo yote ya vita. Wako chini ya shinikizo linaloongezeka kwa sababu tunawaumiza, kuwaondoa makamanda wao wakuu na maelfu ya magaidi. Wako chini ya shinikizo kwa sababu tunabaki thabiti katika malengo yetu, licha ya shinikizo zote."
Huku haya yakijiri shirika la kutetea haki za binaadam la Human Rights watch limesema Hamas iliongoza makundi mengine yenye silaha ya Palestina katika kufanya mamia ya uhalifu wa kivita katika shambulio la ghafla la Oktoba 7 dhidi ya Israel ambalo lilianzisha vita katika ukanda wa Gaza.