Israel yaingia kijeshi Lebanon "kuisambaratisha Hezbollah"
1 Oktoba 2024Maafisa wa jeshi la Israel wamesema oparesheni ya ardhini nchini Lebanon inahusisha uvamizi kwenye maeneo machache ambayo wanasema ni kitisho kwa usalama wa Israel.
Wanajeshi wa Israel walivuka mpaka usiku wa kuamkia leo kuingia Lebanon baadhi wakitembea kwa mguu na wengine ndani ya vifaru vya kijeshi huku ndege za kivita zikifanya mashambulizi ya kusafisha njia.
Katika ujumbe wa video uliotumwa kwa vyombo vya habari, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari, amesema wanajeshi hao wametumwa kwenda kulikabili kundi la Hezbollah kwa dhamira ya kulisambaratisha kundi hilo ili kuwawezesha raia wa Israel kurejea kwenye makaazi yao upande wa kaskazini.
Maelfu ya raia wa Israel wamehamishwa kutoka maeneo yaliyo jirani na mpaka wa Lebanon kutokana na mashambulizi ya kila siku ya maroketi yanayofanywa na kundi la Hezbollah tangu kuzuka kwa vita vya Ukanda wa Gaza kiasi mwaka mmoja uliopita.
"Mashambulizi haya ya ardhini yatazilenga ngome za Hezbollah zinatotishia (usalama) wa miji ya Israel, Kibbutzim na maeneo mengine ya mpakani. Hezbollah imegeuza vijiji vya Lebanon vilivyo karibu na mpaka kuwa kambi zake za kijeshi tayari kuishambulia Israel. Hezbollah imeviandaa vijiji hivyo kama uwanja wa maandalizi ya uvamizi mfano wa ule wa Oktoba 7 kwenye makaazi ya Israel" amesema Hagari.
Hezbollah yashambulia Tel Aviv kwa makombora ya masafa
Hatua hiyo ya Israel kutuma jeshi lake ndani ya Lebanon ilitarajiwa kwa wiki kadhaa sasa baada ya kushuhudiwa mfululizo wa mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la Hezbollah ikiwemo moja lililomuua kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah wiki iliyopita.
Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limeapa kuendelea kupambana dhidi ya Israel na kaimu kiongozi wake alisema hapo jana wamejitayarisha kwa oparesheni ya kijeshi ya ardhini itakayofanywa na Israel.
Mapema leo asubuhi ving´ora vya tahadhari vilisikika mjini Tel Aviv na baadae kukatokea milipuko ambayo jeshi la Israel limesema imetokana na makombora yaliyorushwa kutokea Lebanon.
Kombora moja liliipiga barabara karibu na mtaa wa katikati mwa mji wa Kfar Kassen na duru zinasema mwanamke mmoja amejeruhiwa. Hezbollah imesema ndiyo ilifyetua makombora chapa "FADI 4" hayo kuilenga kambi moja ya kijeshi mjini Tel Aviv.
Hiyo itakuwa ni mara ya pili katika kipindi cha wiki mbili kwa Hezbollah kurusha makombora ya masafa yaliyoulenga na kuufikia mji wa Tel Aviv.
Mataifa kadhaa yaonya kuongezeka uhasama, Marekani yasema Israel ina haki ya kujilinda
Katika hatua nyingine mataifa kadhaa yameelezea wasiwasi wake juu ya kutanuka kwa mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah.
Uturuki imesema hatua ya Israel kutuma jeshi lake ndani ya Lebanon ni kinyume cha sheria ya kimataifa na inakiuka uhuru na hadhi ya mipaka ya nchi hiyo.
Kwa upande wake Urusi imetahadharisha dhidi ya kutanuka uhasama kati ya pande hizo mbili huku Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amehimiza umuhimu wa kutuliza hali ya mambo na kuwalinda raia.
Marekani kupitia baraza lake la usalama wa taifa imesema oparesheni ya Israel ya kuvuka mpaka kuilenga miundombinu ya Hezbollah inakwenda sanjari na haki ya nchi hiyo kujilinda.