1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yahujumu amani Mashariki ya Kati, Mfalme Abdullah

29 Machi 2017

Mfalme wa Jordan Abdullah wa pili ameuambia mkutano wa mataifa ya Kiarabu kwamba amani haiwezi kupatikana katika kanda hiyo bila kuanzishwa kwa taifa la Palestina karibu na Israel.

https://p.dw.com/p/2aG7w
König Abdullah II. bin al-Hussein von Jordanien
Mfalme wa Jordan Abdullah wa pili Picha: Reuters/D. Kitwood

Mfalme Abdullah ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo unaowaleta pamoja viongozi 21 wa kiarabu, amesema azma ya Palestina kuwa taifa linasalia kuwa jambo muhimu zaidi huko Mashariki ya Kati.

Mfalme huyo ameishutumu Israel kwa kuhujumu juhudi za kupata amani kwa kuendelea kujenga makaazi katika ardhi inayohitajika na Wapalestina kwa taifa lao la baadae. Ameongeza kuwa, wataendelea kupinga juhudi zozote za kuwaendea kinyume Wapalestina katika eneo hilo.

Amesema pia mataifa ya Kiarabu yanastahili kuungana na Ulimwengu katika kukabiliana na hatari ya ugaidi.

Israel yastahili kusitisha ujenzi wa makaazi 

"Israel inaendelea upanuzi wa makaazi na suala hilo linakwenda kinyume na juhudi za kupata amani. Hakuwezi kuwa na amani katika ukanda huu bila suluhisho litakalozingatia haki kwa azma ya Waplestina, ambayo ndiyo azma kuu Mashariki ya kati, kupitia suluhu la kuundwa kwa mataifa mawili," alisema mfalme Abdullah.

Katika hotuba yake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameionya Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ambao ni kinyume cha sheria. Amesema suluhu la pekee katika mzozo huo litahakikisha Wapalestina na Waisraeli wanatambua malengo yao na wanaishi kwa amani na kuheshimiana.

Schweiz Genf Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres asema Israel isitishe ujenzi wa makaaziPicha: Reuters/D. Balibouse

Guterres pia amezungumzia mzozo wa Syria katika hiyo hotuba yake.

"Wakati umewadia kuumaliza mzozo wa Syria na nataraji yale mazungumzo ya Astana yanayonuia kusitisha mapigano yatafanikiwa, na tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha mazungumzo hayo ya kisiasa yanayoandaliwa mjini Geneva, yanaelekea katika majadiliano ya kweli," alisema Guterres, "kwa sasa inastahili kuwa wazi kwa wahusika wote kwamba wakati kupambana na ugaidi ni muhimu, mafanikio yoyote  yatadumu kwa mda mfupi tu, iwapo hakutakuwa na suluhu la kisiasa litakalowakubalia wananchi wa Syria kuamua mustakabali wao wenyewe," aliongeza Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Syria Bashar al Assad hakualikwa

Mkutano huu wa mataifa ya Kiarabu umekuja mbele ya mikutano itakayoandaliwa katika ikulu ya White House katika wiki zijazo kati ya rais Trump wa Marekani na viongozi watatu wa Kiarabu, mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi na rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

Trump bado hajabuni sera ya kukabiliana na mzozo huo wa Israeli na Palestina, lakini amesema wazo la kuundwa kwa mataifa mawili linaloungwa mkono kimataifa, sio suluhisho la pekee.

Syiren Präsident Bashar al-Assad Interview
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: Reuters

Wapalestina wanataka kuunda taifa lao katika eneo la Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na mashariki ya Jerusalem katika ardhi iliyonyakuliwa na Israel mwaka 1967, katika yale mapigano ya mashariki ya kati.

Rais wa Syria Bashara al Assad hakuwepo kwenye mkutano huo huko Jordan, kwani hakualikwa ukizingatia kuwa Syria ilisimamishwa kuwa mwanachama wa Muungano huo wa nchi 22 za Kiarabu, kufuatia kule kukabiliana kwa Assad na maandamano dhidi yake mwaka wa 2011, hatua iliyochangia kuanza kwa mapigano nchini humo.

Mwandishi: Jacob Safari/AP/DPA

Mhariri: Daniel Gakuba