1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa

13 Mei 2024

Viongozi wa Israel wameshiriki Siku ya Mashujaa kwa heshima ya wanajeshi waliouawa wakiwa vitani wakati waandamanaji wakimtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kujiuzulu kwa kushindwa kuwaokowa mateka wakiwa salama.

https://p.dw.com/p/4fo0X
Israel Jerusalem | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akihutubia kwenye Siku ya Mashujaa siku ya Jumatatu (Mei 1, 2024).Picha: Gil Cohen-Magen/AP/picture alliance

Sherehe hizo ambazo kawaida hufanyika kwa hamasa ya hali ya juu, mara hii zilitawaliwa na huzuni na hasira juu ya kile wakosoaji wa utawala wa Netanyahu wanachosema ni kushindwa kwake kuzuwia uvamizi wa Oktoba 7, ambapo wapiganaji wa Hamas kutoka Ukanda wa Gaza walivunja seng'enge na kuingia kusini mwa Israel walikosababisha vifo vya watu wapatao 1,200 na kuwachukuwa mateka wengine wapatao 250.

Siku ya Mashujaa ni siku ya mapumziko kwa Israel, ambapo mara ilianza jioni ya Jumapili na  kuendelea hadi usiku wa Jumatatu.

Soma zaidi: Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza

Kwenye uzinduzi wa kumbumbuku hizo katika Mlima Herzi, Netanyahu aliapa kwa mara nyengine tena kwamba atalishinda kundi la Hamas, ahadi ambayo amekuwa akiirejea kila mara ndani ya kipindi cha miezi saba ya vita vikali kwenye Ukanda wa Gaza vilivyoangamiza hadi sasa maisha ya watu 35,000 kwenye Ukanda huo na zaidi ya wanajeshi 600 wa Israel.

"Tumedhamiria kushinda vita hivi, tumewafanya na tutaendelea kuwafanya maadui kulipa gharama kubwa sana kwa matendo yao ya kikatili, tutatimiza malengo ya ushindi, na kubwa zaidi ni kurejea kwa mateka wetu wote nyumbani, ushindi ambao kwa msaada wa Mungu utahakikisha kuwepo kwetu na mustakabali wetu." Alisema Netanyahu.

Wakosoaji wamtaka ajiuzulu

Wakati Netanyahu akihutubia kwenye shughuli hiyo, sauti ya mwanamme mmoja ilisikika ikisema kwa Kiebrania kwamba kauli hiyo ni "takataka" tupu.

Israel Jerusalem | Benjamin Netanyahu
Viongozi wa Israel kwenye Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika Jumatatu (Mei 13, 2024).Picha: Gil Cohen-Magen/REUTERS

Maelfu ya Waisraeili wamekuwa wakiandamana kila wiki kwenye mji wa pwani wa Tel Aviv, wakimtaka Netanyahu ajiuzulu.

Wengi wanaamini alipaswa kuchukuwa hatua zaidi kuhakikisha kuachiliwa salama kwa makumi ya mateka walio kwenye mikono ya Hamas hadi sasa.

Soma zaidi: Mashaka yagubika operesheni ya Israel mji wa Rafah

Netanyahu ameyakataa matakwa ya Hamas ya kukomesha vita hivyo, akisema hatua hiyo italiruhusu kundi hilo kubakia na udhibiti wa Ukanda wa Gaza na pengine kufanya mashambulizi mengine kama ya Oktoba 7.

Hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya Wapalestina 30,000 waliukimbia mji wa Rafah mnamo mwishoni mwa wiki wakati jeshi laIsrael likizidi kujipenyeza kwenye mji huo wa kusini mwa Gaza, ambao linadai ni ngome ya mwisho ya wapiganaji wa Hamas.

Israel pia iliushambulia upande wa kaskazini, ambako baadhi ya wapiganaji wa Hamas wamejikusanya upya licha ya hapo awali jeshi la Israel kudai kuwa lilikuwa limeshalisafisha eneo hilo. 

Idadi ya vifo kwenye Ukanda wa Gaza imeripotiwa hivi leo kupindukia 35,000 huku wengine zaidi ya 75,000 wakijeruhiwa.