Israel: Watu wanane wajeruhiwa mjini Tel Aviv
4 Julai 2023Polisi wa Israel wamesema watu saba wamejeruhiwa kaskazini mwa jiji la Tel Aviv na kwamba mshukiwa huyo aliuawa kwa kupigwa risasi. Mkuu wa polisi, Kobi Shabtai amewaambia waandishi wa habari katika eneo la tukio kuwa mtu huyo alipigwa risasi na raia.
Shambulio hilo limetokea huku wanajeshi wa Israel wakiendelea na operesheni ya kuwasaka wanamgambo wa Kipalestina na silaha katika kambi ya wakimbizi ya Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi. Hadi kufikia sasa Wapalestina 10 wameuawa katika siku ya pili ya operesheni hiyo. Israel imekuwa katika tahadhari ya kutokea mashambulizi ya Wapalestina baada ya kuzindua operesheni kubwa ya kijeshi katika mji wa Jenin kwenye Ukingo wa Magharibi.
Kundi la Hamas, linalotawala katika Ukanda Gaza limeelezea tukio la gari kuwagonga watu huko Tel Aviv kuwa ni jibu la kwanza kutokana na operesheni kubwa ya kijeshi ya Israel katika mji wa Jenin.
Wakati huo huo mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameeleza wasiwasi kutokana na ukubwa wa operesheni inayoendelea katika mji wa Jenin na kwamba upatikanaji wa matibabu umetatizika. Msemaji wa ofisi inayoshughulikia maswala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Vanessa Huguenin, amesema katika taarifa yake fupi kwamba watoto watatu ni miongoni mwa watu waliouawa.
Wanadiplomasia wa nchi za Umoja wa Kiarabu wanakutana leo Jumanne mjini Cairo kuijadili operesheni ya kijeshi ya Israeli katika Ukingo wa Magharibi. Mwanadiplomasia wa Misri anayesimamia Masuala ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Obeida El-Dandarawy amesema Misri inalaani mashambulizi ya Israel.
Ujerumani imesisitiza juu ya haki ya Israel ya kujilinda wakati ambapo inafanya operesheni yake kubwa ya kijeshi kuwahi kutokea katika Ukingo wa Magharibi, lakini imeitaka nchi hiyo izingatie usawa. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema inafuatilia matukio ya ghasia katika eneo hilo kwa wasiwasi mkubwa lakini imesisitiza kuwa Israel kama kila taifa lina haki ya kujilinda dhidi ya ugaidi.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amelihimiza Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kuwalinda raia wa Palestina wakati linapoendesha operesheni yake kubwa kuwahi kutokea katika Ukingo wa Magharibi. Sunak amesisitiza kwamba Uingereza inaunga mkono haki ya Israel ya kujilinda lakini amewaambia wabunge kwamba ulinzi wa raia lazima upewe kipaumbele katika operesheni yoyote ya kijeshi na amezitaka pande zote kuepusha kuongezeka machafuko zaidi.
Vyanzo:DPA/RTRE/AP/AFP