1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Netanyahu aanza zoezi gumu la kuunda serikali

Daniel Gakuba
26 Septemba 2019

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameanza zoezi gumu la kuunda serikali ya muungano wa vyama, baada ya kupata ridhaa ya rais wa nchi hiyo Reuven Rivlin hapo jana, lakini nafasi yake kufanikiwa, ni finyu.

https://p.dw.com/p/3QHK8
Israel Regierungsbildung | Benjamin Netanjahu & Reuven Rivlin
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto) na Rais Reuven RivlinPicha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Netanyahu anazo wiki sita kuanzia sasa za kujaribu kuumaliza mkwamo wa kisiasa unaigubika Israel, lakini hata kwa msaada wa vyama vidogo ambavyo ni washirika wake, bado hawezi kufikisha viti 61 bungeni kumwezesha kuunda serikali. Hali kama hiyo inamkabili pia Benny Gantz, kiongozi wa chama kikubwa cha upinzani cha Buluu na nyeupe.

Wakati wajumbe wa vyama vikuu wakifanya kila juhudi kutafuta suluhisho kabla ya mazungumzo baina yao, kila kimoja kinakilaumu kingine kwa mkwamo uliopo.

Kauli isiyo na matumaini

Kwa kutambua upevu wa kazi inayomkabili, Benjamin Netanyahu hakuwa mwenye matumaini makubwa, alipokubali jukumu la kuunda serikali alilopewa na rais Reuven Rivlin usiku wa kuamkia leo.

''Kwa dhamana uliyonipa, nitafanya kila niwezalo. Nisipofanikiwa, nitarejesha dhamana hiyo kwako, na kwa msaada wa Mungu na wa watu wa Israel na wewe mwenyewe bwana Rais, tutaunda serikali pana ya umoja wa kitaifa.'' Amesema Netanyahu.

Arabische Liste empfiehlt Gantz als Israels Premier | Benny Gantz
Benny Gantz, mkuu wa chama cha Buluu na NyeupePicha: picture-alliance/AP Photo/S. Scheiner

Kikwazo kikubwa ni kuwa Benny Gantz anataka kuiongoza serikali yoyote ya muungano itakayokishirikisha chama chake, na ameapa kuepuka muungano wowote utakaomhusisha Netanyahu akiwa bado anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu.

Hali kadhalika, chama cha Buluu na Nyeupe cha Gantz kinapinga kuingia katika muungano pamoja na vyama vyenye misimamo mikali ya dini ya kiyahudi, ambavyo Netanyahu ameahidi kuwa navyo katika muungano wowote utakaokijumuisha chama chake cha Likud.

Hakuna mwenye ujanja

Mbunge mmoja wa Likud Zeev Elkin, ameiambia redio ya jeshi la Israel kwamba katika mazingira ya sasa kisiasa nchini humo hakuna mwenye ujanja, akisema masharti ya Benny Gantz kumhusu Netanyahu na baadhi ya vyama, hayasaidii chochote mbali na kuielekeza Israel katika uchaguzi wa tatu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Wahlen in Israel - Avigdor Lieberman
Avigdor Lieberman, mwenye ufunguo wa kumaliza mkwamo wa kuunda serikali IsraelPicha: Getty Images/AFP/J. Marey

Lakini hata waziri wa zamani wa ulinzi Avigdor Lieberman ambaye anashikilia ufunguo wa kuutanzua mkwamo uliopo kwa viti vinane vya chama chake, anataka serikali ya muungano inayohusisha vya vikuu viwili, lakini amekataa katakata kushirikiana na vyama hivyo vya kidini, ambavyo Netanyahu amejifungamanisha navyo.

Kwa Netanyahu, suala la kuunda serikali siyo changamoto pekee inayomkosesha usingizi wakati huu, kwani mwendeshamashtaka mkuu wa Israel anakamilisha faili la mashtaka dhidi ya ubadhirifu dhidi yake, ambalo linaweza kuwasilishwa mahakamani katika muda wa wiki chache. Ingawa Netanyahu halazimiki kisheria kujiuzulu baada ya kufunguliwa mashtaka rasmi, hali hiyo ikiokea shinikizo litakuwa kubwa kwake kuweza kulihimili.

 

ape,dpae