Israel kuruhusu misaada ya kiutu kuingizwa Gaza
19 Oktoba 2023Israel imetangaza kuruhusu misaada ya kiutu kuingia Ukanda wa Gaza kutokea nchi jirani ya Misri, wakati ikiendelea na mzingiro wake katika eneo hilo la Wapalestina. Tangazo hilo limetolewa jana na ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mara baada uamuzi wa baraza la mawaziri.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba misaada ya kiutu kwa raia walioko kusini mwa Gaza itaruhusiwa tu endapo haitolifikia kundi la Hamas ambalo linatawala eneo hilo. Tangazo hilo limetolewa wakati Rais wa Marekani Joe Biden akikamilisha ziara yake ambayo ameitumia kutangaza msaada wa Dola milioni 100 za Kimarekani kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Katika hatua nyingine maelfu ya raia katika nchi za Kiarabu na Kiislamu, waliandamana jana kupinga vifo vya mamia ya watu katika shambulizi la hospitali mjini Gaza na kuishutumu moja kwa moja Israel ambayo imekana kuhusika. Israel na wanamgambo wa Hamas wametupiana lawama kwa shambulio hilo la hospitali, huku jeshi la Israel likisema baadaye lilikuwa na "ushahidi" kwamba wanamgambo walihusika.