1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kuchukua jukumu la usalama wa Gaza baada ya vita

7 Novemba 2023

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel itachukua jukumu la usalama wa jumla katika Ukanda wa Gaza kwa muda usiojulikana baada ya vita vyake na Hamas.

https://p.dw.com/p/4YVF9
Palästina Israelische Streitkräfte werfen Leuchtraketen über Gaza-Stadt ab
Anga za Gaza zaendelea kuwaka moto kutokana na makombora ya IsraelPicha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Katika mahojiano na televisheni ya ABC News ya Marekani yaliyoruka Jumatatu usiku, Netanyahu ameonyesha kuwa yuko tayari kuruhusu kusimamishwa mapigano kwa nyakati fulani fulani ili kuwezesha kuachiliwa kwa baadhi ya mateka zaidi ya 240 waliokamatwa na Hamas katika shambulizi lao la Oktoba saba ndani ya Israel, ambalo lilichochea vita hivi mwezi mmoja uliopita. Lakini ameondoa uwezekano wa kuwepo mpango wa usitishwaji kamili wa mapigano bila kuachiliwa huru mateka wote. Netanyahu aliiambia ABC News kuwa Gaza inapaswa kutawaliwa na wale ambao hawafuati mbinu za Hamas.

Soma pia: Guterres: Gaza yageuka uwanja wa makaburi kwa watoto

Waziri mkuu huyo wa Israel alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden jana usiku na Ikulu ya Marekani imesema hapakuwa na makubaliano kuhusu wito wa Biden wa kuwepo na mpango mpana wa kusitishwa vita ili kuruhusu upelekaji wa misaada ya kiutu.

Benjamin Netanjahu
Netanyahu amekataa mpango wa usitishwaji mapiganoPicha: Xinhua/IMAGO

Wapalestina 10,000 wameuawa mpaka sasa

Idadi ya vifo vya Wapalestina imepindukia 10,000. Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na Hamas imesema miongoni mwa vifo hivyo ni watoto 4,100. Zaidi ya watu 2,300 hawajulikani waliko na wanaaminika kuwa wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoharibiwa.

Soma pia: Blinken afanya ziara ya kushtukiza Ukingo wa Magharibi

Wakaazi kaskazini mwa Gaza wameripoti makabiliano makali ya usiku kucha viungani mwa Mji wa Gaza. Wamesema kambi ya wakimbizi ya Shati imepigwa mabomu kutokea angani na baharini kwa siku mbili zilizopita.

Katika upande wa kusini mwa Gaza, ambako Wapalestina wameambiwa watafute hifadhi,shambulizi la Israel la kutokea angani liliharibu makaazi kadhaa mapema leo katika mji wa Khan Younis. Maafisa wa uokozi wameondoa miili ya watu watano kwenye vifusi wakiwemo watoto watatu.

Mjini New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena lilishindwa kukubaliana kuhusu azimio kuhusu vita vya Israel na Hamas. Licha ya zaidi ya saa mbili za majadiliano ya faragha jana, tofauti ziliendelea kushuhudiwa kuhusiana na suala la usitishwaji mapigano kwa ajili ya kuruhusu misaada ya dharura kupelekwa Gaza.

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakaribia mwezi mmoja

UAE kujenga hospitali Gaza

Umoja wa Falme za Kiarabu unaratajiwa kujenga hospitali ya muda katika Ukanda wa Gaza. Shirika la Habari la serikali WAM limesema ndege tano ziliondoka Abu Dhabi kuelekea Arish, kaskazini mwa Misri zikiwa zimebeba vifaa na bidhaa zitakazotumika katika hospitali hiyo ya vitanda 150.

Huku hayo yakijiri, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, ameanza leo ziara ya siku tano katika Mashariki ya Kati ili kushauriana na maafisa wa serikali na asasi za kiraia kuhusu ukiukaji wa haki za binaadamu unaoendelea Gaza kwenye vita vya Israel na Hamas. Turk yuko Cairo leo na kesho Jumatano atazuru Rafah, kwenye mpaka na Gaza, kabla ya kwenda katika mji mkuu wa Jordan Amman Alhamisi.

Wakati huo huo, mamia ya raia wa kigeni na Wapalestina wenye uraia pacha wanaondoka leo katika Ukanda wa Gaza. Karibu watu 150 walio na paspoti ya Ujerumani ni miongoni mwa watu 600 wanaovuka mpaka kuingia Misri. Wengine ni kutoka Romania, Canada, Ukraine, Ufaransa na Ufilipino. Duru za usalama Misri zinasema zaidi ya raia 300 wa kigeni waliondoka Gaza jana, wakiwemo Wamisri 100.

afp, dpa, ap, reuters