1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

12 Aprili 2024

Wasiwasi umeongezeka kufuatia taarifa kwamba Iran inajiandaa kuishambulia Israel ili kujibu tukio la maafisa wake wakuu wa jeshi waliouawa na Israel.

https://p.dw.com/p/4efWQ
Israel
Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha IranPicha: Abir Sultan via REUTERS

Miito ya kimataifa imeongezeka na kuzitaka pande zote kutochokua hatua ambazo zitapelekea kutanuka kwa mzozo katika eneo zima la  Mashariki ya Kati.

Alipotembelea kambi ya jeshi la anga ya Tel Nof kusini mwa Israel, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema hii leo kuwa nchi yake iko tayari kukabiliana na kitisho chochote kutoka kokote:

"Tumo katika nyakati zenye changamoto. Tumo katikati ya vita vya Gaza ambavyo vinaendelea kwa nguvu zote, na wakati huo huo tunaendelea na juhudi zetu za kuwarejesha mateka wetu, lakini pia tunajiandaa na changamoto kutoka kwa mataifa mengine. Tunayo kanuni iliyo wazi kwamba yeyote anayetuumiza, nasi tunamuumiza. Tunajiandaa kukidhi mahitaji ya usalama ya taifa la Israel iwe katika ulinzi au kujihami. Mimi na watu wa Israel tunawaamini na twatarajia kuwa na mafanikio makubwa."

Teheran | Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei Picha: Iranian Leader Press Office/Handout/AA/picture alliance

Israel imekuwa katika hali ya tahadhari kufuatia uwezekano wa shambulio la kulipiza kisasi baada ya mauaji ya jenerali mkuu na maafisa wengine sita wa Iran katika shambulio la anga kwenye ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Damascus mnamo Aprili 1. Israel haikutangaza kuhusika lakini Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema hapo jana kuwa Israel ni lazima iadhibiwe kwa shambulio hilo.

Soma pia: Lufthansa yasitisha safari za ndege za kwenda na kutoka Tehran

Wakati Marekani ikiihakikishia Israel kuwa itasimama upande wake dhidi ya vitisho vyovyote vinavyotolewa na Iran, afisa anayeongoza majeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati, Jenerali Michael Erik Kurilla, amewasili hii leo huko Israel na anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant.

Miito inayozitaka pande zote kujizuia

Berlin-  Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Hossein Amir Abdollahian kuhusu hali ya wasiwasi katika Mashariki ya Kati.

Soma pia: Kiongozi mkuu wa Iran aapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel

Wizara ya Mambo ya Nje imeandika katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter) kwamba ni muhimu kuepuka kuongezeka zaidi kwa mzozo wa kikanda kwa manufaa ya wote na kuwahimiza wadau wote katika eneo hilo kuchukua hatua za uwajibikaji.

Urusi kwa upande wake imetoa wito kwa Iran na Israel kujizuia huku hali ya mizozo na mivutano ikiendelea katika eneo la Mashariki ya Kati. Hayo yakijiri, watu sita wamearifiwa kuuawa katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, kufuatia kile kinachodhaniwa kuwa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel.

(Vyanzo: Mashirika)